News

TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA WAZIRI ULEGA UJENZI BRT AWAMU YA NNE

TANROADS YATEKELEZA AGIZO LA WAZIRI ULEGA UJENZI BRT AWAMU YA NNE

 

 

Dodoma

22 Mei, 2025

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imemuondoa Mhandisi Mkazi wa Mradi wa ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Nne anayesimamia sehemu ya kwanza inayoanzia Maktaba – Mwenge – Ubungo jijini Dar es Salaam, Mhandisi Rajabu Iddi Rajabu kwa kushindwa kumsimamia Mkandarasi na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo.Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia agizo la Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alilolitoa jijini Dar es Salaam tarehe 16 Mei, 2025 baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kubaini uzembe uliosababisha usumbufu katika barabara hiyo ambayo ni kinyume na malengo ya mradi.Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Japherson Nnko ameeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na Mkandarasi anayetekeleza ujenzi huo kufumua barabara katika eneo jipya la Palm Beach, Upanga kabla ya kukamilisha kazi muhimu katika maeneo ya awali ya barabara hiyo kutoka Morocco – Mwenge hadi Nkunda.Mbali na hatua hiyo, TANROADS imefanya maboresho ya usimamizi wa miradi ya BRT Awamu ya Nne na ya kwanza ambapo Mhandisi Allen Natai atasimamia BRT Awamu ya Kwanza wakati Mhandisi Justin Moshi na Mhandisi Issa Mohamed watasimamia BRT Awamu ya Nne lengo likiwa ni kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa na kutekelezwa kwa karibu na ipasavyo.Mhandisi Nnko ametoa rai kwa Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara hasa kwenye maeneo ya Miji yenye changammoto ya msongamano wa magari kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa utaratibu wa kimkataba na kufuata maelekezo ya Mhandisi Mshauri ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kazi zinatekelezwa kwa wakati na ubora ili kupunguza muda wa usumbufu kwa watumiaji wa barabara.Aidha, amewataka Wasimamizi kutoka TANROADS kuhakikisha wanawasimamia Wahandisi Washauri na Makandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu nchini kwa karibu ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezewa kwa wakati uliopangwa.