News

WAZIRI ULEGA AKAGUA MRADI WA BRT 4 – LOT 1, ATOA MAELEKEZO

WAZIRI ULEGA AKAGUA MRADI WA BRT 4 – LOT 1, ATOA MAELEKEZO

 

Dar es Salaam

16/05/2025

Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Ulega, leo Ijumaa Mei 16, 2025, amefanya ukaguzi wa maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Nne, Sehemu ya Kwanza (BRT 4 – Lot 1), unaojumuisha njia kuu kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam kuelekea Mwenge hadi Tegeta, pamoja na sehemu ya Mwenge hadi Ubungo.

 

Katika ziara hiyo, Waziri Ulega ameeleza bayana kuwa na mashaka juu ya namna Mshauri Elekezi anavyotekeleza wajibu wake katika usimamizi wa mradi huo, akionesha kutoridhishwa na uamuzi wa kuanza kazi katika eneo jipya la Palm Beach kabla ya kukamilisha kazi katika maeneo ya Morocco hadi Kaunda.

 

“Nilipopita Palm Beach nimekuta shimo kubwa. Nilipohoji, nikaambiwa mkandarasi ndiye aliyechimba. Swali langu likawa, kwanini aanze huku wakati kule hajakamilisha? Huu ni mtindo unaotatiza sana na unaosababisha misongamano ambayo Mheshimiwa Rais Samia mwenyewe haifurahii,” alisema Waziri.

 

Waziri Ulega ameweka wazi kuwa hali hiyo imempelekea kutoa maagizo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kukusanya taarifa kamili kuhusu Mshauri Elekezi na timu ya wasimamizi ili kufanyiwa uchunguzi wa kina.

 

“Shida si mkandarasi peke yake, shida ni Mshauri Elekezi na baadhi ya wasimamizi wangu. Tunahitaji kujua kwanini wanaweka nguvu eneo moja jipya bila kukamilisha walikoanzia. Hii si kazi ya kubahatisha – lazima kuwe na mpangilio wa kitaalamu,” aliongeza.

 

Waziri Ulega amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, haitavumilia uzembe wala urasimu unaosababisha ucheleweshaji wa miradi ya kimkakati, hasa ile inayolenga kupunguza misongamano ya magari jijini Dar es Salaam.

 

“Mimi kama mwajiri nina mamlaka ya kuwanyang'anya baadhi ya maeneo mkandarasi yeyote au timu yoyote inayoshindwa kwenda na kasi yetu. Haiwezekani mtu anaanza kuchimba eneo jipya kabla ya kumaliza eneo la kwanza. Huu si ufanisi tunaoenda nao,” alisema kwa msisitizo.

 

Waziri pia ameeleza kuwa ipo dalili za baadhi ya watu waliopaswa kusimamia kwa niaba ya Serikali kuonyesha uswahiba na mkandarasi, hali inayoweza kuathiri uwajibikaji.

 

“Nina mashaka Mshauri Elekezi amehamia upande wa mkandarasi badala ya kusimama upande wa mwajiri wake. Kazi yao ni kutushauri sisi, kutulinda na kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa viwango na kwa wakati,” alisema.

 

Kuhusu ucheleweshaji wa mradi, Waziri amewaelekeza wakandarasi waliochelewesha kazi walipe fidia kwa serikali na kwa wananchi kutokana na usumbufu wanaopata kila siku.

 

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa Mradi huo, Rajabu Iddi, ametoa pole kwa wananchi kwa usumbufu unaotokana na ujenzi unaoendelea na kueleza kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati.

 

“Tunajitahidi kadri ya uwezo, akili na juhudi zote kumdhibiti mkandarasi na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati. Tutaendelea kutoa taarifa na kuweka njia za mchepuo kupunguza makali ya msongamano,” alisema Mhandisi Rajabu.

 

Mradi wa BRT 4- Lot 1 unatarajiwa kuwa na vituo 18 vya mwendokasi, ukiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kupunguza adha ya usafiri jijini Dar es Salaam.