News

SERIKALI YAVUNJA MKATABA WA MKANDARASI BARABARA YA TANGA 

SERIKALI YAVUNJA MKATABA WA MKANDARASI BARABARA YA TANGA 

 

Tanga

12/05/2025

Serikali imevunja mkataba na Mkandarasi wa kampuni ya China Railway 15 Bureau Group anayejenga barabara ya Tanga - Pangani - Mkwaja - Bagamoyo (Makurunge), baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba, pamoja na kulipwa kiasi cha shilingi Bilioni 47, ujenzi huo umefikia asilimia 48 pekee.Hatua hiyo imetangazwa tarehe 12 Mei, 2025 na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, wakati wa ziara yake ya kikazi ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa kipande cha barabara hiyo katika Wilaya ya Pangani, Mkoa wa Tanga.

 

Mkandarasi huyo, kampuni ya China Railway 15 Bureua Group anayejenga barabara ya Tanga - Pangani - Mkwaja - Bagamoyo (Makurunge) sehemu ya Tungamaa - Mkwaja - Mkange (km 95.2) wilayani Pangani anadaiwa kushindwa kutekeleza mkataba wa kazi hiyo pamoja na Serikali kumlipa fedha zote kwa wakati.

 

Baada ya kuvunja mkataba wa awali, Waziri Ulega amemuagiza  Katibu Mkuu wa Ujenzi, Balozi Mhandisi Aisha Amour, kuondoa kilometa 25 za barabara hiyo ambazo hajazifanyiwa kazi na badala yake itangazwe zabuni mpya ili wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo wapewe kazi na waanze haraka.

 

Kufuatia agizo hilo, sasa kilometa 25  ambazo hakijaguswa za barabara hiyo na kilometa 70 za barabara inayoanzia Mkange hadi Bagamoyo (Makurunge) zitaunganishwa kwenye zabuni ili apatikane Mkandarasi wa kuijenga.

 

“Mkandarasi huyu ametuangusha na hapa sisi hadai hata senti kwani tushamlipa zaidi ya bilioni 40, yupo nyuma ya muda, vifaa hajavileta vyote, wafanyakazi hawajawaleta wote, hivyo nimechukua maamuzi ya kumnyang’anya sehemu ya kazi ya mradi ili mradi huu ukamilike kwani ni wa muda mrefu na ni kilio cha wananchi wa Pangani na Mkoa wa Tanga kiujumla”, amesisitiza Ulega.

 

Ulega ameendelea kusisitiza kuwa maamuzi hayo ya kumyang’anya mkandarasi sehemu ya kazi ni kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi kwasababu Serikali ingeamua kuvunja mkataba wote ingechukua zaidi ya miezi 6 hadi mwaka mzima mpaka Mkandarasi mpya kupatikana na kuanza kazi, ambapo hasara yake mradi kuendelea kuchelewa.

 

Vilevile, Ulega amemtaka Mkandarasi huyo kuilipa fidia Serikali kwa kuchelewesha mradi huo ambapo ameielekeza timu wa wataalam kuendelea kuchambua kimkataba juu ya hatua zitakazochukuliwa.

 

Ulega amemwagiza Katibu Mkuu huyo kumweka mkandarasi huyo katika orodha ya Wakandarasi wasiofanya kazi vizuri katika miradi ya ujenzi kwa siku za usoni, ili iweze kusadia wakati wa kupata Makandarasi wengine katika miradi mbalimbali ya ujenzi hapa nchini.

 

Kuhusu kilometa 70 ambazo Mkandarasi atatakiwa kuzimalizia, Ulega ameelekeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuisimamia kampuni hiyo ya  China Railway 15 Bureua Group kufanya kazi usiku na mchana, ili  azikamilishe kuzijenga kwa kiwango cha lami ifikapo Oktoba mwaka huu 2025 na endapo watazembea nao watawajibishwa.

 

Kwa upande wake Msimamizi wa mradi huo kutoka TANROADS, Mhandisi Julius Msoffe ameeleza kuwa hadi sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 47.82 ikilinganishwa na mpango kazi wa asilimia 100 na kuongeza kuwa muda wa mkataba wa miezi 36 sawa na asilimia 100 umeisha tangu tarehe 31 Machi 2025.