WAZIRI ULEGA AWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA UJENZI YA MWAKA WA FEDHA 2025/26
Dodoma
05 Mei, 2025
Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Abdallah Hamis Ulega (Mb), leo Mei 04, 2025 amewasilisha bungeni Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/26, ukibeba kaulimbiu ya “Bajeti ya Kazi na Utu”.Katika hotuba yake, Waziri Ulega ameliomba Bunge Tukufu liridhie kupitisha bajeti hiyo jumla ya Shilingi, 2,280,195,828,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.Ambapo kati ya fedha hizo, Shilingi 90,468,270,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara na Taasisi na Shilingi 2,189,727,558,000.00 kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ilikutekeleza miradi ya kimkakati katika sekta ya ujenzi, inayolenga kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.Mhe. Ulega ameeleza kuwa miradi hiyo inaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuleta mapinduzi katika miundombinu nchini.Aidha, Waziri Ulega amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kumuamini na kumteua kushika wadhifa huo tangu Desemba 2024, huku akiahidi kutekeleza majukumu kwa moyo na uaminifu kwa kushirikiana na watendaji wa wizara hiyo.Katika hotuba hiyo pia, Waziri Ulega ametoa pongezi kwa viongozi wakuu wa serikali akiwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu na Bunge zima kwa ushirikiano na miongozo inayosaidia utekelezaji bora wa majukumu ya wizara.