SERIKALI YAWAPA FURSA YA MIRADI WAKANDARASI WAZAWA-ULEGA
Dodoma
05 Mei, 2025
Wakandarasi wazawa nchini wamepata neema kubwa kufuatia uamuzi wa Serikali kuongeza ukomo wa thamani ya kazi wanazoweza kupewa moja kwa moja kutoka Shilingi bilioni 10 hadi bilioni 50. Hatua hii imeelezwa kuwa ya kimapinduzi katika kukuza uwezo wa ndani, kuongeza ajira na kuimarisha mzunguko wa fedha ndani ya nchi.Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/26 leo Mei 05, 2025, Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Abdallah Ulega amesema uamuzi huo umetokana na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha imani kwa wakandarasi wazawa si kwa misingi ya kizalendo pekee bali kwa uwezo wao wa kiutendaji ulioanza kung’ara.“Baadhi ya kampuni za nyumbani zimeonyesha uwezo mkubwa unaofanana na wakati mwingine hata kuzidi wajenzi kutoka nje,” alisema Waziri Ulega mbele ya Bunge.Aidha, Waziri huyo ameeleza kuwa katika mpango wa matengenezo ya dharura ya barabara kutokana na athari za El Niño na Kimbunga Hidaya, kati ya mikataba 81 iliyosainiwa yenye thamani ya Shilingi bilioni 556.9, mikataba 72 imetekelezwa na wakandarasi wazawa – hatua inayoashiria imani kubwa ya Serikali kwa kampuni za ndani.Waziri Ulega pia amezitaja baadhi ya kampuni zilizong’ara na kufanikisha miradi mikubwa kuwa ni pamoja na ESTIM, Nyanza Road Works Ltd, Hari Singh & Sons Ltd, Mlumangi Construction Co. Ltd, ROCKTRONIC Ltd na nyinginezo.Hatua hii imepokelewa kwa shangwe na wadau wa sekta ya ujenzi, wakiamini itatoa nafasi zaidi kwa kampuni za kizalendo kukuza mitaji yao, teknolojia, na kutoa ajira kwa vijana wengi wa Kitanzania.