RAIS MWINYI AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA BARABARA YA KIBADA–MWASONGA–KIMBIJI (KM 41)
Dar es Salaam
25 April, 2025
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo Ijumaa Aprili 25, 2025 ameongoza hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa barabara ya Kibada–Mwasonga–Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41 kwa kiwango cha lami, ikiwa ni sehemu ya kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanzania.
Katika hotuba yake, Dk. Mwinyi amesisitiza umuhimu wa mradi huo kwa ustawi wa wananchi wa Kigamboni na taifa kwa ujumla, akitoa wito kwa Wizara ya Ujenzi na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, kwa mujibu wa mkataba na kwa viwango vya ubora vinavyokubalika.
“Ni wajibu wa wananchi kushirikiana na mkandarasi katika kulinda vifaa vya ujenzi ili mradi huu ukamilike kama ulivyopangwa,” amesema Dk. Mwinyi huku akibainisha kuwa maendeleo ya miundombinu kama haya ni ushahidi wa mafanikio ya Muungano ndani ya miaka 61.
Ameongeza kuwa amani na mshikamano uliopo kati ya pande mbili za Muungano ndio msingi wa utekelezaji wa miradi mikubwa kama huu, akisisitiza umuhimu wa kudumisha hali hiyo hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa aliyemwakilisha Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetekeleza miradi mingi ya barabara nchi nzima, huku barabara ya Kibada–Mwasonga–Kimbiji ikitajwa kuwa ya kimkakati kwa ajili ya kukuza uchumi wa Kigamboni.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuleta neema ya maendeleo mkoani humo na kusisitiza kuwa barabara hiyo ni kiungo muhimu cha uchumi wa Kigamboni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta ameeleza mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Estim Construction kwa gharama ya Shilingi bilioni 83.8 na unatarajiwa kukamilika Disemba 2025, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 30 hadi sasa.
Mradi huo tayari umezalisha ajira 331, kati ya hizo 326 ni Watanzania na 5 ni raia wa kigeni. Serikali inaendelea kushughulikia ombi la mkandarasi kuhusu nyongeza ya muda wa miezi mitano kufuatia changamoto za kimkataba.
Barabara hiyo inatarajiwa kuongeza ufanisi wa usafiri Kigamboni, kuvutia uwekezaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.