BILIONI 100 KUJENGA MADARAJA BARABARA YA KUSINI - MAKALLA
l UJENZI WA DHARURA WA MADARAJA HAUTAATHIRI BAJETI - ULEGA
l BUNGE LAIPONGEZA TANROADS KWA KURUDISHA MAWASILIANO LINDI
Lindi
09 April, 2025
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla amesema Serikali imetenga kiasi cha zaidi ya Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja matano kwenye maeneo korofi ya barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kusini.
Makalla ameyasema hayo ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara mkoani Lindi ambapo pamoja na mambo mengine alipita katika Kata ya Somanga Mtama iliyopo katika Jimbo la Kilwa Kaskazini mkoani Lindi kwa ajili ya kusalimia wananchi wa eneo hilo na kujionea mwenyewe maendeleo ya ukarabati wa dharura wa barabara iliyoharibiwa na mvua.
Makalla aliyefuatana na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni sikivu na inajali maisha na maendeleo ya watu na ndiyo sababu imeamua kuwekeza kiasi hicho kwa ajili ya ujenzi wa madaraja hayo muhimu ili kufanya barabara hiyo muhimu ipitike kwa majira yote ya mwaka.
“Nimepita hapa kuja kusalimia wananchi na kujionea mwenyewe maendeleo ya matengenezo ya barabara hii ambayo yaliathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi. Serikali ya Rais Samia itatumia zaidi ya shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya kukarabati madaraja hayo,”alisema.
Kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kumpongeza Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, watendaji wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na watumishi wa wizara ya ujenzi waliohusika na ukarabati kwa kujenga maeneo hayo kwa weledi, kasi kubwa na kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha mawasiliano kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Kusini yanarejea.
“Nakupongeza sana ndugu yangu Ulega, kwa weledi mkubwa uliouonyesha kwa kuweza kurudisha mawasiliano hayo kwa muda mfupi na napenda kukwambia kuwa unatakiwa kuwa mkali pale uzembe unapotendeka kwani kile anachokifanya ni kwa maslahi ya CCM kwa sababu ndicho chama chenye dhamana kwa wananchi.
Kabla ya Makalla kuzungumza, Ulega alimpa taarifa fupi ya maendeleo ya ukarabati unaoendelea ambao hata hivyo alisema hautaathiri ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya madaraja katika maeneo korofi ya barabara na kumshukuru Rais Samia, ambaye ni pia ni Mwenyekiti wa CCM, kwa kuhakikisha fedha za kutosha zinatengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Kwa upande wake Waziri Ulega amesema ujenzi wa madaraja matano kwenye barabara kuu ya Dar es Salaam - Lindi yanayoendelea hakutaathiri juhudi za sasa za kukarabati maeneo yaliyoharibiwa na mafuriko ya mvua katika siku za karibuni.
Ulega alitumia fursa hiyo kutangaza pia kwamba serikali tayari imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja ya kudumu na ni kazi endelevu hadi itakapokamilika. Eneo la Somanga na Matandu mkoani Lindi linafanyiwa ukarabati wa dharura baada ya barabara hiyo kuharibiwa na mvua.
“Tutambue kuwa ujenzi wa madaraja sio suala la wakati mmoja ni la hatua kwa hatua. Niwatoe hofu Watanzania kwamba toka ilipotokea dharura mwaka jana ya kukatika maeneo hayo Serikali imechukua hatua madhubuti na kila mahali yupo Mkandarasi anafanya wajibu wake”, amesisitiza Ulega.
Ulega amewashukuru wananchi wote waliokumbwa na changamoto hiyo kwa uvumilivu na subira pamoja na kuwapongeza Wakandarasi na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kushiriki zoezi hilo usiku na mchana ili kuhakikisha mawasiliano yanarajea.
Nalo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limeipongeza Serikali na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kwa kuchukua hatua za haraka kurejesha mawasiliano kwenye barabara ya Kusini.
Akizungumza Bungeni, Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, amesema hatua zilizochukuliwa za kurejesha mawasiliano zimepunguza mateso kwa wananchi na kuruhusu kuendelea kwa shughuli za uchumi.
Tangu kuharibiwa kwa barabara hiyo kutokana na mvua zillizosababisha mafuriko, Ulega na watendaji kutoka Wizara ya Ujenzi na TANROADS waliweka kambi katika maeneo ya Somanga Mtama na Matandu ili kurejesha usafiri katika hali ya kawaida.
Naibu Spika pia amewapongeza mawaziri wote walioshiriki katika kuhakikisha mawasiliano yanarejea kwa wakati.