News

WAHANDISI WANAWAKE TANROADS DODOMA WASIMAMIA VYEMA MIRADI YA KIMKAKATI

WAHANDISI WANAWAKE TANROADS DODOMA WASIMAMIA VYEMA MIRADI YA KIMKAKATI

 

Dodoma,

07 Machi, 2025

Wahandisi wanawake wa Wakala ya Barabara Tanzania  (TANROADS) Mkoa wa Dodoma wanasimamia vyema miradi ya kimkakati iliyopo kwenye mpango wa serikali, ambayo kukamilika kwake itachangia kukua kwa uchumi wa nchi kutokana na sekta ya usafiri na usafirishaji kuimarika.

 

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 07 Machi, 2025 na Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya sherehe za Wanawake Duniani ambazo zitahitimishwa tarehe 08 Machi, 2025 kitaifa zitafanyika mkoani Arusha, ambapo kaulimbiu ni “Wanawake na Wasichana 2025: Tumairishe Haki, Usawa na Uwezeshaji”.

 

Mha. Zuhura amesema kwa mkoa wa Dodoma wanatekeleza miradi 40 ambayo inashirikisha wahandisi wanawake wakishirikiana na wanaume waliopo katika kada hiyo, ambapo jumla wanawatumishi 100 na kati yao 30 ni wanawake.

 

“Ninajivunia kuwa mhandisi na jukumu langu ni kusimamia miradi mikubwa na hata midogo, ambapo katika mwaka huu wa fedha kwa mkoa wetu tuna miradi mingi kama 40 midogo na mikubwa ya kimkakati, ambayo kwa kiasi kikubwa tunaisimamia vizuri tukijiamini kabisa na kile tunachofanya, na ili kufikia kwenye kiwango kizuri,” amesema Mha. Zuhura.

 

Amesema wahandisi wanasimamia hatua kwa hatua miradi yote ya miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali zinatumika vyema katika malengo yaliyokusudiwa, licha ya kuwa na wakandarasi,  kwa kuwa baada ya kukamilika itakabidhiwa mkoa ambao ndio waendeshaji na wasimamizi.

 

 

Mha. Zuhura ametoa wito kwa wanawake kuwa wajibidishe kwenye kazi mbalimbali kwani serikali imewajengea mazingira rafiki katika utendaji kazi, ambazo zitawaletea kipato, akitoa mfano kwenye ujenzi wa miundombinu kumekuwa na wanawake wakifanyakazi katika idara mbalimbali ikiwemo uendeshaji wa mitambo ya ujenzi, kwenye uongozi.

 

 

“Naona fahari kuwa mhandisi mwanamke, ambaye nilianzia chini kama mhandisi wa kawaida na sasa nimefikia kwenye nafasi ya umeneja, kwa kushirikiana na watumishi wenzangu, nawahamasisha wanawake wenzangu tufuate malengo yetu bila kukata tamaa,” amesema Mha. Zuhura.

 

Pia amewataka wanafunzi kujiwekea nia ya kuwa wahandisi kuanzia shule ya msingi kwa kupenda masomo ya sayansi na kuweka bidii watafanikiwa katika malengo yao.

 

Mha. Zuhura ameishukuru Sretkali ya Awamu ya Sita iliyopo chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini na kuwekeza kwa kutoa fedha nyingi za ujenzi wa miundombinu ya mkoa wa Dodoma, ambao ndio makao makuu ya nchi.

 

MWISHO