BILIONI 6.5 KUTUMIKA, MRADI WA UJENZI WA DARAJA LA KIGOMBO
Lindi
16 Februari, 2025
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imetekeleza ahadi yake kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi kwa kuanza ujenzi wa Daraja la Kigombo lenye urefu wa mita 25, baada ya daraja la awali kusombwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya.
Mradi huu, unaogharimu shilingi bilioni 6.5, unatekelezwa kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi na ukisimamiwa na Kitengo cha Engineering Consulting Unit (TECU) kutoka TANROADS kama Mhandisi Mshauri, Mradi huu unahusisha pia ujenzi wa madaraja madogo mawili (box culverts) ili kuimarisha barabara ya Kilanjelanje – Nanjilinji – Namichiga – Ruangwa.
Hayo yamesemwa na na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Nzengo na kubainisha kuwa, daraja litakuwa na nguzo kubwa mbili (abutments) zenye misingi 10 kila upande, kila msingi ukiingia chini kwa mita 20 ili kuhakikisha uimara wake wa kudumu.
Kwa mujibu wa Meneja wa Mradi, Athumani Mohamed Twahir, kutoka Macapo Construction and General Supplier, ujenzi unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 10, huku matarajio yakiwa ni kufikia Agosti mwaka huu na kuahidi kuwa, kazi itafanyika kwa viwango vya juu na kwa wakati, akisema "hatutamuangusha Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa imani waliyoonyesha kwa wakandarasi wazawa."
Daraja hili litasaidia wakulima wa mazao ya biashara kama ufuta, mihogo, mananasi na korosho kusafirisha mazao yao kwenda Kilwa na Ruangwa, hivyo litakuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto ya usafiri, hasa wakati wa mvua. Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara nchini, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuinua uchumi na ustawi wa wananchi.
Wananchi wa Lindi wametakiwa kuwa wavumilivu wakati ujenzi huu ukiendelea, kwani serikali tayari imeshapata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hiyo.