News

SERIKALI KUTEKELEZA KWA AWAMU UJENZI BARABARA YA BUKOMBE – KATORO

SERIKALI KUTEKELEZA KWA AWAMU UJENZI BARABARA YA BUKOMBE – KATORO

 

Dodoma

29 Januari, 2025 Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema inatekeleza Ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Bukombe – Katoro ( km 58.20) kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo Awamu ya kwanza inahusisha sehemu ya Bukombe (Ushirombo) hadi Bwenda (km 5.3) ambapo zabuni za kumpata Mkandarasi zimefunguliwa tarehe 20 Januari, 2025 na kazi ya tathmini ya zabuni hizo inaendelea.  

Hayo yameelezwa leo Januari 29,2025 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Rose Busiga aliyeuliza ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Barabara ya Bukombe hadi Katoro kwa kiwango cha lami.


Kadhalika, Serikali inatekeleza Ujenzi wa Barabara ya Katumba – Mbambo – Tukuyu (km 83) kwa awamu.  Sehemu ya kutoka Lupaso hadi Mbambo (km 20) ambapo kutoka Kabanja hadi Tukuyu (km 7) ujenzi kwa kiwango cha lami umekamilika.

  Sehemu iliyobaki ya kutoka Katumba – Lupaso (km 35.3) na Mbaka – Kibanja (km 20.7) mikataba ya ujenzi imesainiwa na kwa sasa mkandarasi yupo kwenye maandalizi ya kuanza kazi baada ya kulipwa malipo ya awali na kusisitiza kuwa kazi zimepangwa kukamilika mwezi Mei, 2027 kwa sehemu zote mbili.

Mha. Kasekenya amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Rungwe Albert Mwantona aliyeuliza lini Serikali itamaliza ujenzi wa Barabara ya Katumba – Mbambo – Tukuyu. Kuhusu Ujenzi wa Barbara ya Old Korogwe - Kwamndolwa – Magoma – Mashewa – Bombomtoni – Maramba hadi Mabokweni amesema kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Kina wa barabara (km 127.69) iko katika hatua za mwisho ambapo kwa sasa Mhandisi Mshauri anafanya kazi ya kugawa Barabara katika sehemu nne kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji.

   Mha. Kasekenya ameeleza hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Mjini Dkt. Alfred Kimea aliyeuliza ni lini ujenzi wa Kiwango cha lami Barabara ya Old Korogwe - Kwamndolwa – Magoma – Mashewa – Bombomtoni – Maramba hadi Mabokweni utaanza.