News

MRADI WA UWANJA WA NDEGE WA MSALATO KUKAMILIKA KWA VIWANGO VYA KIMATAIFA

MRADI WA UWANJA WA NDEGE WA MSALATO KUKAMILIKA KWA VIWANGO VYA KIMATAIFA

 

Dodoma

26 Januari, 2025

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati inafanyika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.

Moja ya miradi hiyo ni ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ambao unatajwa kuwa lango muhimu la kiuchumi na maendeleo kwa taifa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta amesema hayo hivi karibuni na kusisitiza kuwa, uwanja huo umejengwa kwa viwango vya kimataifa vya Shirika la Usafiri wa Anga la Kimataifa (ICAO) ukizingatia vigezo vya usanifu vilivyopo kwenye ambatisho la 14 (Annex 14).

Mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Msalato umegawanywa katika sehemu mbili kuu ambapo kila sehemu ina umuhimu mkubwa katika kufanikisha malengo ya kuwa na uwanja wa kisasa na wa kimataifa.

Sehemu ya kwanza inajumuisha ujenzi wa maeneo ya matembezi ya ndege (movement areas) ikiwa ni pamoja na njia ya kuruka na kutua ndege runway yenye urefu wa kilomita 3.8 inayokidhi viwango vya viwanja vyote duniani, barabara za maungio (Taxiway) na maegesho ya ndege (aprons).

Hadi sasa utekelezaji wa sehemu ya kwanza umefikia asilimia 84 Inatarajiwa kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili 2025 sehemu hii itakuwa imefikia hatua muhimu ya kukamilika (significant completion) hali itakayowezesha baadhi ya shughuli kuanza kufanyika.

Gharama za ujenzi wa sehemu hii pekee zimefikia shilingi bilioni 165.

Sehemu ya pili ya mradi inahusisha ujenzi wa majengo mbalimbali yakiwemo jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 1.5 kwa mwaka huku likiwa na uwezekano wa kupanuliwa kadri mahitaji yatakavyoongezeka, jengo la kuongozea ndege, kituo cha kuzalisha umeme (power station) na majengo mengine muhimu kwa uendeshaji wa shughuli za uwanja huo.

Kwa sasa utekelezaji wa sehemu ya pili ya mradi umefikia asilimia 52 huku gharama zake zikifikia shilingi bilioni 192.