News

BASHUNGWA ATAKA KASI UJENZI WA BARABARA YA NYAMWAGE - UTETE IONGEZEKE

BASHUNGWA ATAKA KASI UJENZI WA BARABARA YA NYAMWAGE - UTETE IONGEZEKE

Rufiji

24 Oktoba, 2024

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ametaka kuongezwa kwa kasi ya ujenzi wa barabara ya Nyamwage - Utete (km 33.7) inayojengwa kwa kiwango cha lami na Mkandarasi China Railway Seventh Group (CRSG), na kukamilisha kuleta Wataalam pamoja na mitambo itakayowawezesha kutekeleza mradi huo kwa wakati na kwa mujibu wa mkataba.

 

Bashungwa ametoa agizo hilo leo Oktoba 24, 2024 Wilayani Rufiji Mkoani Pwani wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, ambayo hajaridhishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi huyo ambaye hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia saba (7) pekee.

 

“Meneja wa TANROADS hakikisha unamsimamia Mkandarasi huyu kama mikataba inavyosema, nitarudi hapa kukagua nataka nione timu yote ya wataalam wakiwa wamejipanga pamoja na vifaa vya kazi vikiwa site vinaendelea na kazi, hiyo siku ukiwa hujasimamia basi sintasinta kuondoka nawewe Dodoma”, amesisitiza Bashungwa.

 

Bashungwa ameeleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaiwezesha Wizara ya Ujenzi fedha za ujenzi wa barabara hiyo ambapo Mkandarasi hadai malipo kwa sasa kwa hiyo hana sababu yoyote ya msingi ya kutoongeza kasi ya ujenzi wa barabara hiyo.

 

Aidha, Bashungwa amemtaka Mkandarasi CRSG kujitathimini kutokana na kusuasua mara kwa mara katika baadhi ya miradi ya ujenzi wa barabara ikiwa ni pamoja na iliyopo kwenye mikoa ya Mara, Katavi, Ruvuma, Dar es Salaam na Pwani.

 

Aidha, Bashungwa ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo ili iweze kukamilika kwa wakati.

 

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameidhinisha kuanza kwa maandalizi ya ujenzi wa barabara mpya yenye Km 354 inayotoka Chalinze - Magindu- Bwawa la Mwalimu Nyerere - Utete.

 

Nae, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Pwani Mha. Baraka Mwambage ameahidi kumsimamia mkandarasi huyo ili aweze kuongeza kasi katika ufanyaji  kazi kwa wastani wa asilimia 8 kwa mwezi ambapo sasa anafanya kazi wastani wa asilimia 2.1 kwa mwezi.