News

TANROADS YAELEZA MAFANIKIO KATIKA MKUTANO WA 17 WA TATHMINI YA SEKTA YA UCHUKUZI

TANROADS YAELEZA MAFANIKIO KATIKA MKUTANO WA 17 WA TATHMINI YA SEKTA YA UCHUKUZI

Arusha

23 Oktoba, 2024
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeeleza mafanikio yake kwenye Mkutano wa 17 wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Sekta ya Uchukuzi unaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 23 hadi 25 Oktoba, 2024.

Kupitia mkutano huo TANROADS imeeleza namna ilivyofanya ukarabati wa miradi 26 ya miundombinu ya barabara yenye jumla ya urefu wa kilomita 893.93 kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu wa TANROADS, Mhandisi Ephatar Mlavi, akiwasilisha tathmini hiyo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu, Mhandisi Mohamed Besta, amesema kuwa miradi ya kimkakati kama daraja la J.P. Magufuli (Kigongo-Busisi) lenye urefu wa mita 3,200 linalovuka Ziwa Victoria, jijini Mwanza, ipo kwenye hatua ya mwisho ya ujenzi, ikiwa imekamilika kwa asilimia 93 pamoja na barabara unganishi yenye urefu wa kilomita 166 imejengwa sambamba na daraja hilo.

Mhandisi Mlavi pia ameeleza kuhusu maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, ambapo barabara ya kuruka na kutua ndege imefikia asilimia 72.59 ya ukamilishaji, na jengo la abiria limefikia asilimia 39.42.

Kwa upande mwingine, amesema kuwa TANROADS inaendelea kutekeleza miradi ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PPP), ikiwemo ujenzi wa barabara ya Kibaha-Chalinze (km 78.9), Chalinze-Morogoro (km 84.9) na Morogoro-Dodoma (km 250). Aidha, ukamilishaji wa barabara za Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) jijini Dar es Salaam na uboreshaji wa viwanja vya ndege pia ni sehemu ya vipaumbele vya TANROADS.

Hata hivyo, Mhandisi Mlavi amekiri kuwa changamoto za upungufu wa fedha na uwezo mdogo wa wakandarasi wa ndani zimeathiri baadhi ya miradi.

Hata hivyo, changamoto hizo zimepatiwa ufumbuzi kupitia mikopo ya ujenzi na ushirikiano wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PPP).

Pia, TANROADS imekuwa ikiwawezesha wakandarasi wa ndani kwa kuwapa kazi za matengenezo na ukarabati.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Massawe, amemweleza Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati alipotembelea banda la TANROADS, kwamba taasisi hiyo inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 37,225.72.

Mhandisi Massawe amebainisha mafanikio ya ujenzi wa madaraja kama Tanzanite, Mfugale, na Kijazi jijini Dar es Salaam, na kuongezea kuwa ujenzi wa daraja la Jangwani unatarajiwa kuanza hivi karibuni baada ya kusainiwa kwa mkataba.

Aidha, TANROADS imepanga kujenga daraja kubwa eneo la Kikavu mkoani Kilimanjaro, na miradi ya barabara kama awamu ya pili ya Arusha-Moshi-Holili (km 11) kutoka Tengeru hadi USA River, pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa Manyara.

Katika kulinda barabara zake, TANROADS imeweka mizani 16 ya kupima magari yakiwa kwenye mwendo, hatua iliyosaidia kupunguza msongamano wa magari barabarani.