News

WAZIRI DKT. MWIGULU AIELEZEA TANROADS KUENDELEA KUTOA ELIMU KWA WATUMIAJI JUU YA MATUMIZI YA BARABARA

WAZIRI DKT. MWIGULU AIELEZEA TANROADS KUENDELEA KUTOA ELIMU KWA WATUMIAJI JUU YA MATUMIZI YA BARABARA

Arusha

12 Septemba, 2024

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema, kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ya kuboresha na kujenga miundombinu bora ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini, elimu ya matumizi yake inapaswa kuendelea kutolewa kwa watumiaji ikiwemo wenye vyombo vya moto na watembea kwa miguu, ili ufanisi na tija ya maboresho hayo iweze kupatikana.

Miongoni mwa miundombinu hiyo ni ujenzi wa barabara ya njia nne na sita katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kupunguza msongamano na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Amesema hayo Septemba 12, 2024 katika kuhitimisha Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki jijini Arusha, ambapo amesisitiza kuwa, uwepo wa barabara hizo ni jambo jipya hivyo suala la elimu kwa watumiaji ni jambo linalopaswa kutiliwa mkazo.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Udhibiti wa Mikataba wa TANROADS, Mhandisi Mussa Madirisha Kaswahili amesema, kupitia kongamano hilo wameweza kubadilishana uzoefu wa matumizi ya mfumo wa kieletroniki katika kufanya manunuzi pamoja na kujadili changamoto ambazo zimewahi kuwakumba nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kuzindua mifumo yao na baadaye kufikia maamuzi ya kuondoa changamoto hizo.

Vilevile Mhandisi Madirisha amebainisha kuwa, mambo mengi yamezungumzwa katika kongamano hilo ikiwa ni pamoja na mafanikio kwenye sekta ya manunuzi kwa kupitia mifumo ya kidijitali na hatimaye kufikia malengo ya uwazi, uwajibikaji na kupunguza mlolongo kwenye suala la ununuzi.

"Mambo mengi yamezungumzwa ikiwa ni mafanikio ya sekta ya manunuzi kwa njia ya kidijitali ambapo suala la uadilifu, uwazi, uwajibikaji na kupunguza mlolongo wa ununuzi likitiliwa mkazo ili kuweza kukidhi matakwa na mahitaji ya nchi, ambapo asilimia kubwa bajeti ya serikali takribani asilimia 60 hadi 70 inatumika kwenye suala la ununuzi" alisema Mhandisi Madirisha na kusisitiza

…"Kwa hiyo ni eneo nyeti sana ambalo linapaswa kutiliwa mkazo ili kuweza kufikia azma ya Serikali ambayo inakusudiwa, kwa sababu manunuzi yanayofanyika yanakwenda kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya kimkakati na ya Kitaifa ambayo inalenga kuwainua na kuwaondolea wananchi changamoto ambazo wanazo".

 

Aidha, Afisa Manunuzi, Bi Maria Silayo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Fedha ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kuja na mfumo wa NeST ambao unawezesha manunuzi hivi sasa kufanyika kwa njia ya kidijitali na kuondoa kero zilizokuwepo hapo awali wakati manunuzi yalikuwa yakifanyika bila mfumo.

Kongamano la 16 la Ununuzi wa Umma la Afrika Mashariki lilioanza Septemba 09, 2024 na kuhitimishwa Septemba 12, 2024 jijini Arusha lilikuwa na kaulimbiu inayosema "Digitalization For Sustainable Public Procurement" (Matumizi ya Dijitali kwa Ununuzi wa Umma Endelevu), na nchi zilizoshiriki ni pamoja na mwenyeji Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini na Uganda, ambao wamepata fursa ya kujadili na kubadilishana uzoefu katika sekta ya ununuzi wa umma katika ukanda huo.

Kongamano hilo lilifunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kufungwa na Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, ambapo pia mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya umma wa NeST (National - e - Procurement System) ulizinduliwa rasmi.


Katika kongamano hilo TANROADS ilitunukiwa tuzo kutokana na ushiriki wake  wa kufanikisha kufanyika kwa kongamano hilo muhimu kwa mustakabali wa sekta ya manunuzi kwa manufaa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia kupitia banda la Wakala katika kongamano lilitoa elimu mbalimbali ikiwemo matumizi ya barabara, hifadhi ya barabara, kwa watu waliotembelea banda hilo pamoja na kueleza majukumu ya Wakala na kazi zake za kila siku hapa nchini.