NAIBU WAZIRI WA UJENZI AIPONGEZA TANROADS ALIPOTEMBELEA BANDA LAO KATIKA MAONESHO YA NANENANE
Dodoma
08 Agosti, 2024
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Geofrey Kasekenya, amewataka wanaopewa dhamana ya kujenga miundombinu ya barabara kuzingatia ubora na thamani ya fedha.
Mha. Kasekenya, amesema hayo leo tarehe 8 Agosti, 2024 alipotembelea banda Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), lililopo katika maonyesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
"Rai yangu kwa wanaopewa dhamana ya kutengeneza barabara wahakikishe kwamba wanasimamia ubora wa barabara na thamani ya barabara kwa kuwa wataalam tunao na vifaa vya kisasa tunavyo", amesema Mha. Kasekenya.
Aidha, amesema hategemei kuona wataalamu walio na ujuzi na vifaa vya kisasa, lakini bado barabara zinaharibika kabla ya wakati.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwekeza fedha nyingi kwenye ununuzi wa vifaa vya kisasa vya ujenzi wa barabara nchini.
"Serikali imewekeza kiasi kikubwa sana cha fedha ili kupata vifaa ambavyo vitasaidia kupata miundombinu bora ya barabara nchini" amesema Mha. Kasekenya.
Kadhalika, amesema TANROADS, hivi sasa inavifaa vya kisasa vinavyotumika kwenye ujenzi wa barabara ikiwemo vifaa vya kupima ubora wa udongo.
"Kuna mitambo ambayo inatumika kupima ubora wa udongo kuangalia ni udongo upi unafaa kwa ajili ya kubeba mizigo itakayokuwa inapita juu ya barabara,".
Mha. Kasekenya ameongeza kuwa "Hapo pia wanamitambo ambayo inauwezo wa kuangalia kila tabaka la barabara linahitaji udongo upi na uwe na ubora upi kwa kila hatua inayofika na hata mitambo yao inaweza kuonyesha tabaka zote zikishakamilika kama zimejengwa kwa kiasi na kiwango kinachotakiwa" amesema Mha. Kasekenya.
Amesema pia wanayomitambo inayoweza kupima kama kuna mipasuko ambayo maji yanaweza kupenya na kuharibu ubora wa barabara na kupunguza ubora wake vilevile kuna mtambo ambao unauwezo wa kupima barabara inayobonyea ambayo inaweza kusababisha ajali au magari kutotembea katika hali ya usalama.
Alimalizia kwa kutoa wito kwa wakazi wa Dodoma na mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kwenda kwenye banda la TANROADS, ili kujifunza teknolojia mbalimbali na kuona uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya ujenzi nchini.