RAIS SAMIA AWEKA WAZI MKAKATI WA KUUFUNGUA MKOA WA MOROGORO KWA BARABARA
Morogoro
04 Agosti, 2024
Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara yenye urefu wa Kilometa 66.9 kwa kiwango cha lami pamoja na daraja la Mto Ruaha Mkuu lenye urefu wa mita 133, Serikali ya Awamu ya Sita imeahadi kuendelea na ujenzi wa vipande vingine vya barabara lengo likiwa ni kuunganisha mkoa wa Morogoro na mikoa inayopakana nayo.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Agosti 04, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa upanuzi wa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Kilombero, Wilayani Kilombero mkoani Morogoro.
Dkt. Samia amesema, mikoa ya Morogoro, Njombe na Ruvuma ni miongoni mwa mikoa ambayo inazalisha chakula kingi hivyo uwepo wa miundombinu bora utarahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao ya chakula na kufikisha katika soko kwa wakati.
"Mikoa ya Morogoro, Njombe na Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayozalisha chakula kingi hivyo tunataka kuiboresha miundombinu ili kuhakikisha chakula kinachozalishwa kinafika kwenye soko" alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
Sambamba na hilo, Dkt. Samia ametoa shukrani zake kwa wafadhili waliochangia katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidatu hadi Ifakara ambao ni Jumuiya ya Umoja wa nchi za Ulaya (EU), Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na Shirika la Misaada La Uingereza (UKAID).
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaeleza wananchi kuwa, katika ziara yake mkoani Morogoro pia analenga kuangalia maeneo yaliyoathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha na kuangalia namna ya kufanya marekebisho au kujenga upya miundombinu iliyoathiriwa.
Katika kutekeleza hilo Rais Dkt. Samia amesema "Fedha kwa ajili ya kazi hiyo iko tayari na pia nimetoa maagizo kwa Waziri wa Ujenzi pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, na maeneo mengine kazi imeshaanza na maeneo mengine kazi zitaanza mara moja."