TANROADS NA MHANDISI ELEKEZI WAKUTANA KUWEKA MIKAKATI YA KUHAKIKISHA MRADI WA IRINGA - KILOLO (KM 33.6) UNA KAMILIKA KWA WAKATI
Iringa
10 Julai, 2024
Kufuatia kuanza kwa kusua sua kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Iringa hadi Kilolo yenye urefu wa kilometa 33.6, Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeingilia kati suala hilo na kuchukua hatua za makusudi ili kuhakikisha kasi ya utekelezaji wa mradi unaendana sawa na muda pamoja na mpango wa utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha kwamba unakamilka kwa muda ulipangwa.
Moja ya hatua zilizochukuliwa na Wakala (TANROADS) kukutana na kufanya kikao cha pamoja na mkandarasi anayetekeleza mradi huo kampuni ya China Henan Engineering company pamoja na mhandisi mshauri kampuni ya RV Associates kutoka nchini India na kisha kuweka mikakati ya pamoja ili utekelezaji wa mradi uendane sawa na mpango wa awali wa utekelezaji wa mradi huo.
Hayo yamesemwa Julai 09, 2024 na Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS Mhandisi Japherson Nnko alipotembelea mradi huo ambapo amesisitiza kuwa, moja ya sababu kubwa ya kuutembelea mradi huo ni kuona namna ya kuusukuma ili utekelezaji wake uende kwa kasi na haraka zaidi.
"Tumefanya mazungumzo na yalituhusisha sisi TANROADS, mkandarasi pamoja na mhandisi mshauri, na tumeweka mikakati ya pamoja. Na kama tutakwenda vizuri basi ndani ya miezi miwili hadi mitatu ijayo tunaamini, utakelezaji wa mradi utarudi katika hatua za utekelezaji ambazo ni sawa sawa na mpango wa awali ambao leo tulipaswa kuwa asilimia zaidi ya 10." alisema Mhandisi Nnko na kuongeza
"Tumekubaliana kwamba tutaendelea na mpango huo mkakati wa kuharakisha utekelezaji wa mradi, hivyo tunaamini tutafanikiwa kurudi katika mpango wa awali na kuanza kutekeleza kwa kasi ambayo imekusudiwa, hivyo mradi utatekelezwa na kukamilika ndani ya muda uliokusudiwa wa miezi 24 (miaka miwili) "
Mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Iringa hadi Kilolo yenye urefu wa kilometa 33.6 ulianza kutekelezwa mnamo tarehe 29 Januari, mwaka huu ikiwa ni moja ya miradi ambayo inatekelezwa na serikali ikishirikiana na Benki ya Dunia (WB) kupitia Program ya Roads to Inclusion and Social Economic Opportunities (RISE), ambapo kukamilika kwa barabara hii kutaleta ufanisi mkubwa katika sekta ya usafirishaji.