UJENZI WA UWANJA WA NDEGE IRINGA KUKAMILIKA AGOSTI 30, 2024 WAZIRI MKUU AISIFU TANROADS NA WIZARA YA UJENZI KWA USIMAMIZI MZURI
Iringa
08 Julai, 2024
Mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Iringa ulipo kata ya Nduli mkoani Iringa umefikia asilimia 93, ambapo unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Agosti, 2024 ukitajwa kukuza na kufungua zaidi fursa mbalimbali ikiwemo za kiuchumi na kiutalii.
Hayo yamesemwa Julai 08, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa alipotembelea na kukagua mradi huo ambapo ameeleza kuridhishwa na utekelezaji huku akitoa pongezi kwa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) pamoja na Wizara ya Ujenzi kwa usimamizi mzuri wa mradi.
Sambamba na hilo, Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza Wizara ya Ujenzi kupitia timu yake ya watalaamu kufanya kikao cha pamoja na idara, taasisi pamoja na mkandarasi anayetekeleza mradi huo kwa ajili ya maandalizi ya kuanza kutumika uwanja huo mapema ifikapo Septemba Mosi, mwaka huu.
"Wizara ya Ujenzi kupitia timu yenu ya watalaamu muitishe kikao cha pamoja na watalaamu kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA), Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Shirika la Ndge (ATCL), TANROADS, mkandarasi pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama kujadili maandalizi ya kutumika kwa uwanja wa ndege ifikapo Septemba Mosi, 2024. Tunataka Septemba Mosi, 2024 ndege iweze kutua" alisema Waziri Mkuu
Vilevile ametumia fursa hiyo kutangaza neema ya ujio wa ujenzi wa viwanja vya ndege katika mikoa ambayo haina viwanja hivyo ili kurahisisha na kuboresha huduma kupitia usafiri wa anga.
Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Simiyu, Lindi, Njombe na Tanga ambapo amesema mikoa hiyo itapata viwanja vya ndege na kufanya kila mkoa nchini kuwa na uwanja wake wa ndege na hivyo safari za ndege kwa kila mkoa zitakuwepo.