News

"MENEJA TANROADS KIGOMA ATOA UFAFANUZI KUHARIBIKA KWA BARABARA KIPANDE CHA MITA 50 ENEO LA BUSUNZU"

"MENEJA TANROADS KIGOMA ATOA UFAFANUZI KUHARIBIKA KWA BARABARA KIPANDE CHA MITA 50 ENEO LA BUSUNZU" 

Kigoma

26 Machi, 2024

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma Mha. Narcis K. Choma ametoa ufafanuzi kuhusu kipande cha video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha kuharibika kwa kipande cha mita 50 eneo la Busunzu kwenye  barabara kuu ya kutoka Kigoma kwenda Mwanza.

 

Amesema uchunguzi wa awali kuwa unaonesha kuwa barabara hiyo imepatwa na kitu kinaitwa landslide (kushuka kwa kipande kikubwa cha ardhi) na matatizo ya mabadiliko ya kimazingira (Geo-environmental) ambayo yanahitaji uchunguzi mkubwa zaidi wa kina ambao unaendelea hivi sasa.

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari Habari leo tarehe 26 Machi 2024; Meneja huyo ameeleza TANROADS ilishapata taarifa na kuanza kuchukua hatua "tangu tarehe 24 mwezi wa pili 2024 tulipewa taarifa na Mhandisi Mshauri akishirikiana Kampuni ya Kitanzania kwamba wameanza kuona mipasuko katika barabara kwenye eneo hilo la Busunzu tukawashauri waendelee kuiangalia’’

 

“Baada ya siku mbili wakasema wanaona mipasuko ile inaongezeka kila kukicha, TANROADS tulichukua hatua ya kuhusisha kitengo chetu cha uchunguzi wa kimahabara na nyenzo ili wafanye uchunguzi wa kina kwa sababu wao wanavyovifaa vya kisasa vya kuweza kujua shida ni nini, tukaona ni vema vilevile kutumia Taasisi nyingine nje ya TANROADS kwa hivyo tumealika taasisi inayofanya uchunguzi wa kihandisi kutoka Chuo kikuu cha Dar- es Salaam ili kujua tatizo ni nini’’. ameeleza.

 

Amesema “tumeona kufumua hiyo sehemu na kujenga upya kuna hatari ya kutokea tena mipasuko kama hiyo ambapo kwa kuwa barabara hiyo ilishaanza kutumika Mkandarasi Mshauri amelekezwa afunge eneo hilo lisiendelee kutumika kwa sababu linaweza kuwa hatari kwa watumiaji wa barabara, kwa sasa magari yanapita kwenye barabara pembeni kwa hiyo barabara imeendelea kupitika kama kawaida.

 

Amesema usanifu ambao ulifanyika katika barabara hiyo ulionesha eneo hilo la Milima lazima likatwe kupunguza mlima uliokuwepo na ilifanyika hivyo walipima uwezo wa udongo na kuweka matabaka yote kama inavyotakiwa.

 

 Ameongeza kuwa kama uchunguzi utaonesha ni makosa ya Mkandarasi au ni makosa ya kiutendaji hatua stahiki zitachukuliwa “Wananchi wa Kigoma wasiwe na wasiwasi tutaendelea kufuatilia kwa karibu kujua tatizo ni nini ili tulitatue tupate barabara ambayo ni bora na yenye viwango’’.