News

TANROADS kufanya usanifu wa kina eneo korofi la daraja la mto Dumila

TANROADS kufanya usanifu wa kina eneo korofi la daraja la mto Dumila

 

Morogoro

Februari 28, 2024

 

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kufanya usanifu wa kina katika eneo korofi la daraja la mto Dumila, barabara kuu ya Morogoro – Dodoma ili kujenga miundombinu ambayo itakuwa ni suluhu ya kudumu katika eneo hilo ambalo kipindi cha mvua kubwa kama za El - nino hujaa maji na kutishia kukata mawasiliano ya barabara.

Hayo yameelezwa tarehe hivi karibuni  kwenye ziara ya Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa Mkoani Morogoro ambaye alitembelea na kukagua miundombinu ya daraja lililopo kwa sasa ambalo licha ya jitihada za mara kwa mara zinazofanywa na Serikali kupitia TANROADS za kuzibua, kuondoa taka ngumu, udongo na mchanga eneo hilo bado limeendelea kuwa korofi hasa kipindi cha mvua kubwa.

Waziri Bashungwa ameelekeza Watalaam wa TANROADS wakati huu wa usanifu waangalie uwezekano wa kujenga daraja la dharura wakati ujenzi wa daraja la kudumu ambalo litaweza kwenda na mahitaji ya eneo hilo ukiendelea bila kuchepusha barabara na kwenda kudhoofisha uchumi wa mji wa Dumila.

Ameeleza “Mtendaji Mkuu wa TANROADS Usanifu ambao mmesema unaisha Aprili 2024, uzingatie marekebisho na maelekezo ambayo tumeyatoa baada ya kutembelea daraja hili, upo uwezekano tukajenga daraja la muda huku tukijenga daraja la kudumu vizazi na vizazi katika eneo hili bila kuhamisha barabara na hizo kilomita huko juu, na kusumbua uwekezaji mkubwa wa Kijamii ambao umeshafanywa na Serikali katika mji wa Dumila’’.

Amesema pia Serikali imekusudia kutafuta fedha kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 15 kuanzia Kingolwira – Morogoro Mjini mpaka Kihonda ili kupunguza tatizo la msongamano hasa pale magari yanapoharibika yanashindwa kuegeshwa pembeni kwa sababu hakuna nafasi.

Vile vile Waziri Bashungwa amesema katika eneo la Mtanana barabara kuu ya Morogoro – Dodoma tayari Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha usanifu umekamilika, na sasa zinakwenda kujengwa kilomita sita kwa kuinua barabara na kuweka Makalvati makubwa ili hata mvua kubwa zitakaponyesha mawasiliano ya barabara yasikatike eneo hilo.