News

GOVERNMENT SIGNS SEVEN CONTRACTS VIA EPC+F ARRANGMENT

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TANROADS imesaini mikataba mikubwa ya kujenga kwa kiwango cha lami Barabara 7 zenye jumla ya km 2,035 kwa kutumia Utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC + F),

Akizungumza wakati wa zoezi la kutia saini mikataba hiyo lililofanyika leo tarehe 16 juni, 2023 Jijini Dodoma
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema ni mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kuwa na miradi mikubwa yenye jumla ya kilometa 2,035 ambayo itaanza kutekelezwa kwa wakati mmoja katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema Mikataba saba (7) ya ujenzi iliyosainiwa leo itagharimu jumla ya Shilingi za Kitanzania Trilioni 3.775 na inatarajiwa miradi yote itekelezwe na kukamilika ndani ya miaka mitano (5).

Ametaja barabara ambazo zitajengwa kwa utaratibu huu wa EPC + F ni: - Barabara ya Kidatu – Ifakara – Lupiro – Malinyi – Kilosa Kwa Mpepo – Londo – Lumecha/Songea (km 435.8); Barabara ya Arusha – Kibaya – Kongwa (km 453.42); Barabara ya Handeni – Kiberashi – Kijungu – Kibaya – Njoro – Olboroti - Mrijo Chini – Dalai – Bicha – Chambolo – Chemba – Kwa Mtoro – Singida (km 384.33); Barabara ya Igawa – Songwe – Tunduma (njia nne) (km 237.9).

Nyingine ni Barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale (km 175); Barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa (km 339) ; na Barabara ya Mafinga – Mtwango – Mgololo (km 81).

Waziri Prof. Mbarawa amefafanua kuwa madhumuni ya ujenzi wa barabara hizo ni kuboresha mtandao wa barabara nchini na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji ili kuchochea uzalishaji, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa wananchi kwa sehemu zinazopita barabara hizo na kwa Taifa kwa ujumla.

Akitoa taarifa fupi ya mikataba hiyo Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta amesema kupitia Utaratibu wa EPC+F, Makandarasi watawajibika kufanya usanifu wa kina (Design) na kujenga barabara hizo kwa viwango na ubora ulioainishwa kwenye Mikataba, Vihatarishi vyote (risk) vinavyohusu usanifu wa mradi na muda wa ujenzi vitabebwa na Mkandarasi, hivyo, utaratibu huo utawezesha Makandarasi kusanifu na kujenga barabara kwa Viwango na teknolojia za kisasa.

Amesisitiza kuwa (TANROADS) itasimamia ujenzi wa barabara hizo kwa mujibu wa vigezo na masharti yaliyopo kwenye mikataba, ambapo Makandarasi watakuwa na timu nne (4) kwa kila mradi mkubwa ili kuharakisha utekelezaji wa Miradi hiyo Hivyo, sehemu zote zitaanza kutekelezwa sambamba kwa wakati mmoja na kwa utaratibu huo, kazi zitafanyika kwa umakini na kukamilika mapema.

"Nitoe wito kwa Makandarasi kufanya kazi zao kwa weledi wa hali ya juu ili kazi zote zikamilike ndani ya muda uliopangwa kwa viwango na gharama zilizokubalika." Ameongeza Mhandisi Besta.