News

TANROADS YAENDELEA KUJENGA UWEZO WA WATUMISHI KATIKA MATUMIZI YA MFUMO WA e-MREJESHO

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uendeshaji katika Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Elirehema Saiteru amesema mfumo wa Mawasiliano wa e - mrejesho umeiwezesha wakala kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo kuongeza uwazi, uwajibikaji na utawala bora kwa kusikiliza maoni na kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi.               

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo ya kuimarisha mfumo wa e - mrejesho kwa watendaji wake ndani ya wakala yaliofanyika mjini Morogoro ,Saiteru amesema ili TANROADS iweze kukidhi mahitaji ya wadau wake ni muhimu ikawekeza kwenye mfumo huo ili iweze kujitathmini na kubaini mapungufu yaliyopo hatua itakayosaidia kuweka mifumo rafiki ya utoaji haki kwa wananchi inaowahudumia.                          

Amesema kwa TANROADS matumizi ya mfumo wa e - mrejesho yanasaidia kuiunganisha Wakala na wananchi inaowahudumia na kuwapa fursa ya kutoa maoni na kuwasilisha malalamiko yao jambo ambalo limesaidia kubaini mahitaji na mapungufu yaliyopo na hivyo kuweka mikakati ya kuyatatua.            

Aidha Saiteru ameongeza kuwa mfumo huo ni nyenzo muhimu kwa TANROADS katika utekelezaji wa dhana ya Utawala bora kwa kutoa fursa kwa wananchi kutoa maoni na malalamiko yao na baadae kufuatilia na kufahamu hatua zilizochukuliwa kuthibitisha kiwango cha uwajibikaji ndani ya wakala.                

Amesisitiza kuwa ili mfumo huo utoe majibu chanya kwa taasisi, ni muhimu kila mtumishi kuwajibika kujibu kero au hoja iliyoelekezwa kwake kwa wakati ili wananchi walioiwasilisha wasiachwe na maswali bila majibu.              

Kaimu Mkurugenzi Saiteru alihitimisha hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyowahusisha wakuu wa idara kutoka mikoa yote na makao makuu, maafisa rasilimali watu na wasimamizi wa vitengo vya mizani, matengenezo na mipango kuzingatia matumizi sahihi ya teknolojia ili kuuwezesha mfumo huo kufanya kazi kwa ufanisi.