Waziri wa Ujenzi, Masanja Kadogosa, ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara zitakazotumika wakati wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mkoani Arusha, unaosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia Kitengo cha TECU.
Waziri Kadogosa ametoa pongezi hizo leo, Novemba 23, 2026 wakati wa ziara yake mkoani Arusha ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo, ambapo ameipongeza TANROADS kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Amesisitiza umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa barabara hizo ndani ya muda uliopangwa ili kurahisisha usafiri na usafirishaji kuelekea katika uwanja wa AFCON.
Aidha, amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi kwa kuhakikisha kazi zinafanyika saa 24, mchana na usiku, ili kutumia ipasavyo muda uliopo na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Hata hivyo, Waziri Kadogosa amesisitiza kuwa kasi ya utekelezaji wa kazi hizo haipaswi kuathiri ubora wa ujenzi. Ameitaka TANROADS kuendelea kufanya usimamizi wa karibu ili kuhakikisha viwango na ubora unaotakiwa vinazingatiwa katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kufuatilia maendeleo ya miradi ya miundombinu ya barabara na kuhakikisha inakamilika kwa wakati, kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa na kwa manufaa ya wananchi pamoja na watumiaji wengine wa barabara hizo.