Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imesisitiza umuhimu wa wahandisi wasimamizi wa miradi kutumia maarifa wanayopata kupitia mafunzo kazi katika kuboresha utendaji wao, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha matokeo chanya yanapatikana katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza katika mafunzo kazi kwa Wahandisi Wasimamizi wa Miradi wa TANROADS Mwaka 2026 (TANROADS Project Engineers Excellency Retreat 2026) yanayofanyika jijini Arusha, Afisa Rasilimaliwatu Mwandamizi na Mratibu wa Mafunzo wa TANROADS, Agness Nalitolela, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwaimarisha washiriki hao katika maeneo ya uongozi, usimamizi wa rasilimaliwatu, uwajibikaji na weledi.
Amesema mafunzo hayo yanatarajiwa kuwawezesha wahandisi kusimamia watumishi walio chini yao kwa ufanisi, kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi na kuhakikisha majukumu ya usimamizi wa miradi yanafanyika kwa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma.
Nalitolela amesema matarajio ya mafunzo hayo ni kuhakikisha maarifa yanayotolewa na kujadiliwa darasani yanageuzwa kuwa matokeo halisi katika maeneo ya kazi, huku rasilimali za Umma zikilindwa na kusimamiwa ipasavyo.
Vilevile amewataka washiriki kutumia fursa hiyo kwa kuyafanyia kazi maarifa wanayopata, akisisitiza kuwa mwajiri ametumia muda na rasilimali katika kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na uadilifu.
Halikadhalika amesisitiza kuwa, mafanikio ya mafunzo hayo hayatapimwa kwa ushiriki wa darasani pekee, bali kwa namna Wahandisi watakavyotumia maarifa hayo kuleta matokeo chanya katika utendaji wao wa kila siku.