News

TANROADS YAUNGANISHA WAHANDISI NA UONGOZI KUDHIBITI VIHATARISHI KATIKA MIRADI

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imewakutanisha wahandisi wasimamizi wa miradi, viongozi wa taasisi na watendaji kutoka kurugenzi mbalimbali katika mafunzo kazi kwa waandishi wasimamizi wa miradi yanayolenga kuimarisha usimamizi wa miradi na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri utekelezaji wake.

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uendeshaji wa TANROADS, Elirehema Obed Saiteru, amesema mafunzo hayo yamelenga kujenga mazingira ya kubadilishana uzoefu, kushauriana na kujifunza baina ya watendaji wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi.

Amesema uamuzi wa kuandaa mafunzo hayo umetokana na tathmini za ndani za taasisi pamoja na mrejesho kutoka kwa wadau mbalimbali, zilizobainisha maeneo yenye changamoto na udhaifu unaohitaji kufanyiwa maboresho.

Saiteru amesema tofauti na kutegemea mafunzo yanayotolewa kwa kukaa darasani pekee, TANROADS imeona umuhimu wa kuwapa watendaji wake nafasi ya kujadili changamoto zinazojitokeza katika utendaji wa kila siku na kutoa mrejesho wa ndani unaoweza kusaidia kuongeza ufanisi.

Ameeleza kuwa hayo pia yanahusisha wataalamu kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Tume ya Maadili, watakaotoa mada zinazohusiana na usimamizi wa vihatarishi katika miradi.

Aidha, amesema majadiliano hayo yatatoa fursa kwa kurugenzi mbalimbali kubainisha maeneo ambayo yanahitaji maboresho katika uratibu na utekelezaji wa majukumu, ili kuondoa ucheleweshaji na vikwazo vinavyoweza kujitokeza.

Amesema kikao hicho cha siku tatu kilichoanza Jumatano, Novemba 18, 2026, kinatarajiwa kuhitimishwa Ijumaa, Novemba 20, 2026, kwa maazimio yatakayowezeshwa kupitia mpango kazi maalumu kwa ajili ya utekelezaji wa maboresho yatakayokubaliwa.