Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imelenga kuongeza tija na kuboresha matokeo ya miradi ya ujenzi wa barabara kupitia kuimarisha usimamizi wa miradi, kwa kuwashirikisha wahandisi, mameneja wa miradi na wataalamu wanaohusika na uandaaji wa miradi hiyo.
Akizungumza katika Mafunzo kazi ya Wahandisi wasimamizi wa Miradi(TANROADS Project Engineers Excellence Retreat) jijini Arusha, Mhandisi Ephatar Mlavi, Mkurugenzi wa Mipango ya Miundombinu TANROADS, amesema mafunzo hayo yanalenga kutathmini utendaji wa wahandisi, kubaini maeneo ya maboresho na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi.
Amesema mafunzo hayo pia yanatoa fursa kwa washiriki kutathmini mafanikio yaliyofikiwa, kujadili changamoto zinazojitokeza na kuweka mikakati ya kuzitatua, kwa lengo la kuimarisha ufanisi katika usimamizi na utekelezaji wa miradi.
Vilevile Mhandisi Mlavi ameeleza kuwa, kama ilivyo katika shughuli nyingine za kiutendaji, usimamizi wa miradi unakabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo kukutana kwa pamoja kunatoa nafasi ya kuzijadili na kutafuta njia za kuzitatua au kuboresha mifumo ya utendaji.
Amesisitiza kuwa matarajio ya kikao hicho ni kuona maboresho katika utendaji kazi wa wahandisi, wasimamizi wa miradi pamoja na wataalamu wanaohusika na uandaaji wa miradi, hatua itakayochangia kuongeza tija katika usimamizi na matokeo ya miradi ya TANROADS.