News

MWISHO WA ENZI ZA KUJIFUNGULIA KWENYE MTUMBWI, DARAJA LA MITOMONI LAGEUKA KUWA MKOMBOZI WA AFYA NA UCHUMI RUVUMA

Wananchi wa Kijiji cha Mitomoni, mkoani Ruvuma, wamesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara na Daraja la Mitomoni umekuwa mkombozi kwao kwa kuondoa adha ya kuvuka mto kwa kutumia mitumbwi na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya, usafiri na shughuli za kiuchumi.

Mkazi wa kijiji hicho, Eliza Kibona, amesema kabla ya daraja hilo wanawake wajawazito walikabiliwa na changamoto kubwa ya kufika kwenye huduma za afya, hali iliyosababisha baadhi yao kujifungulia kwenye mitumbwi na wengine maeneo ya barabarani kutokana na ugumu wa usafiri.

Amesema kwa sasa hali imebadilika kwani usafiri umekuwa rahisi na wananchi wanaweza kufika kwenye huduma za afya ndani ya saa moja na nusu hadi mbili, huku akitoa shukrani kwa Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo.

Naye Samwel Brazio amesema awali wananchi walilazimika kuvuka mto kwa msaada wa watu na kutumia mitumbwi wanapohitaji kwenda hospitalini au maeneo mengine, lakini daraja hilo limeondoa changamoto hiyo na kurahisisha safari zao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mitomoni, Ally Mpaiche, amesema upatikanaji wa usafiri umeimarika, tofauti na awali ambapo magari yalikuwa na ratiba chache, huku kwa sasa wananchi wakipata huduma za usafiri nyakati tofauti.

Naye Emmy Mohamed amesema daraja hilo limeimarisha biashara kwa kuwezesha bidhaa kufika kwa wakati bila kuharibika, hasa kipindi cha masika ambacho awali kilikuwa changamoto kubwa kwa wafanyabiashara.

Akizungumzia huduma za usafirishaji, Afisa Usafirishaji Patrick Akitanda amesema kampuni yao imewekeza magari mawili, likiwemo basi aina ya Yutong lenye siti 40 na bus aina ya Tata, ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Mitomoni na Songea Mjini.

Wananchi hao wamesema daraja hilo limeimarisha mawasiliano kati ya kijiji cha Mitomoni na Songea Mjini, na kufungua fursa zaidi za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.