News

BARABARA KUENDELEA KUKARABATIWA MARA KWA MARA – DKT. MSONDE

Wizara ya Ujenzi nchini imeweka mikakati ya kufanya ukarabati wa mara kwa mara kwa miundombinu ya barabara, ili ziendelee kutumiwa na wananchi kwa maendeleo ya taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 16 Novemba, 2026 jijini Mwanza kwenye Mkutano wa 19 wa tathmini ya Utendaji wa Sekta ya Uchukuzi (JTRS) unaojumuisha wadau wa Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, TAMISEMI na TARURA.

Dkt. Msonde amesema mkutano huu unajipambanua kwa ukubwa na kutathmini walipotoka, walipo na wanapokwenda katika masuala ya miundombinu, ambapo pia wanapitia changamoto za miundombinu zilizojitokeza kwa kipindi cha mwaka mzima na kupatiwa ufumbuzi kupitia machapisho mbalimbali yaliyowasilishwa.

Akizungumzia barabara ambazo zipo chini ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Dkt. Charles Msonde amesema kuwa sasa kunamtandao wa barabara zaidi ya Kilometa 37,000 na zipo kwenye barabara Kuu na za Mkoa, ambapo kati ya hizo Kilometa 12,000 ni za lami na nyingine ni za changarawe na udongo.

Amesema ni wajibu wa sekta ya ujenzi kuangalia namna ya kuziondoa barabara zisizokuwa na lami na kuangalia namna bora ya kuzitunza zenye lami ili ziendelee kudumu kwa muda mrefu, kwa kuwa barabara zinamuda maalum wa kuishi.

“Barabara zinatakiwa kufanyiwa ukarabati wa mara kwa mara ili zeindelee kudumu kwa muda mrefu, kwa kuwa zinamuda maalumu wa kuishi kama vile binadamu anamwisho wa maisha, hivyo ili iendelee kuwa bora inatakiwa kuboreshwa zaidi ili iwe imara,” amesema Dkt. Msonde.

Amesisitiza kuwa barabara sio kitabaka pekee cha lami, bali ni msingi wa matabaka mengi ambayo yanatumiwa na wataalam ili kuzuia maji, ambayo ni adui wa barabara yasiingie kuiharibu matabaka ya barabara.

Amesema mbali na mtandao wa barabara, pia kuna korido tisa za barabara ambazo zimegawanywa kwa ajili ya kuhudumiwa kirahisi.

Halikadhalika, ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kufanya makubwa kwa kufanikisha sasa fedha za matengenezo ya barabara zinakwenda moja kwa moja kwenye mifuko ya barabara, ambapo inarahisisha matengenezo yanakwenda kwa kasi. Mkutano huo umefunguliwa na Waziri Mkuu, Mhe. Mwigulu Nchemba.