Ujenzi wa barabara ya Mingoyo–Masasi yenye urefu wa kilomita 118.2 mkoani Lindi umefikia asilimia sita, huku kazi za awali zikiendelea ikiwemo usafishaji wa zaidi ya kilomita 45 na maandalizi ya ujenzi wa daraja la Nyangao.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi, Mhandisi Ezra Magogo Daniel, amesema uchunguzi wa kitaalamu wa udongo (Geotechnical Investigation) katika eneo la daraja la Nyangao umeanza na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Amesema mradi huo unatekelezwa na kampuni ya China Communications Construction Company Limited (CCCC) kwa gharama ya Sh bilioni 212.3 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2027.
Ameeleza kuwa barabara hiyo ni sehemu muhimu ya Ushoroba wa Mtwara unaounganisha Mtwara na Songea kupitia Masasi, ikiwa na mchango mkubwa katika kurahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka migodi ya mikoa ya Ruvuma na Songea kwenda Bandari ya Mtwara.
Aidha, amesema barabara hiyo itarahisisha usafirishaji wa saruji kutoka kiwanda cha Dangote kwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ikiwemo Ruvuma, Njombe na Mbeya, pamoja na nchi jirani za Zambia na Kongo.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Daniel amewataka watumiaji wa barabara hiyo na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani kuwa wavumilivu wakati ujenzi ukiendelea, kutokana na changamoto za kutumia njia za michepuko katika baadhi ya maeneo.
Vilevile ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa uwekezaji huo utaboresha miundombinu ya usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi.