News

RC SHIGELA ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA BARABARA YA DAREDA–DONGOBESH

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martine Shigela, ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Dareda Center–Dareda Mission yenye urefu wa kilomita saba, unaotekelezwa na mkandarasi kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering Group kutoka China.

Shigela ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea mradi huo kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wake katika sehemu ya kwanza ya mradi wa barabara ya Dareda–Dongobesh yenye jumla ya urefu wa kilomita 60.

Mradi huo umegawanywa katika sehemu mbili, ambapo sehemu ya kwanza ni Dareda Center–Dareda Mission yenye urefu wa kilomita saba, huku sehemu ya pili ikiwa ni Dareda Mission–Dongobesh yenye urefu wa kilomita 53.

Ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji pamoja na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya za Mbulu na Babati.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Ofisi ya Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Manyara, kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mradi huo katika sehemu ya kwanza.