Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Njombe imeimarisha mikakati ya kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño, kwa kuweka nguvu katika ulinzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara kabla na wakati wa msimu huo wa mvua unaotarajiwa kudumu kwa takriban miezi nane.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Njombe, Mhandisi Kipembawe Msekwa, amesema maandalizi hayo yanahusisha ushirikiano na wadau mbalimbali, utekelezaji wa maelekezo kutoka Makao Makuu ya TANROADS pamoja na usambazaji wa vifaa muhimu vya kukabiliana na changamoto za mafuriko na mmomonyoko wa udongo.
Amesema ofisi hiyo imepokea na kusambaza kalavati za chuma (CMP), gabions na magodoro maalumu (mattresses) katika maeneo yanayohitaji hatua za kuimarisha miundombinu.
Katika hatua nyingine, TANROADS imeweka kipaumbele katika Barabara ya Makambako–Songea kwa kufanya matengenezo ya viraka, usafishaji wa mitaro na surface dressing (uwekaji wa tabaka jipya) katika maeneo ya Kifanya, Agha Filo hadi Makambako.
Pia, kazi za kuimarisha barabara na kingo za mito zinaendelea katika maeneo ya Daraja la Halali, Kitulo, Ndulamo, Mkongwa na Kibena–Lupembe. Katika Barabara ya Njombe–Makete–Kikondo, hatua za kuchonga maeneo yenye milima mikali, kujenga kalavati na kuweka gabions zinachukuliwa kupunguza uwezekano wa maporomoko ya ardhi.
Aidha, katika Daraja la Mto Rumakali, mikakati ya kuzuia maji kuathiri barabara inahusisha uwekaji wa vikapu vya mawe (gabions) kwa ajili ya kuinua na kuimarisha tuta.
Mhandisi Msekwa amewataka wananchi kuwa sehemu ya mapambano dhidi ya athari za mvua za El Niño kwa kutoa taarifa mapema wanapoona maji yakivuka juu ya barabara na kuepuka kupita katika maeneo hayo.
Vilevile, amewakumbusha wakulima wanaolima pembezoni mwa barabara kutokata miti hovyo wala kuacha matawi yanayoweza kuziba njia za maji, hali inayoweza kuchangia mafuriko.