Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Manyara, inaendelea na matengenezo na ukarabati wa Barabara Kuu ya Gehandu–Babati (T014), kwa lengo la kuboresha miundombinu, kuimarisha usalama na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo.
Kazi hizo zinazotekelezwa kwa awamu zinahusisha uwekaji wa tabaka jipya la lami (Resealing), matengenezo makubwa ya viraka (Intensive Patching) na ukarabati wa sehemu zilizoharibika.
Katika kipande cha Gehandu hadi Miny'engi chenye urefu wa kilometa 15, Mkandarasi kampuni ya SAIMOO Limited amekamilisha kwa asilimia 100 uwekaji wa tabaka jipya la lami, huku akiendelea na awamu ya pili ya kilometa 20 kutoka Miny'engi hadi Katesh.
Katika awamu hiyo ya pili, mkandarasi amekamilisha uwekaji wa tabaka jipya la lami katika kilometa 1.8 na matengenezo makubwa ya viraka katika kilometa 14, huku utekelezaji wa mkataba wake kwa ujumla ukiwa umefikia asilimia 21.
Wakati huo huo, Mkandarasi kampuni ya Rocktronic Ltd anaendelea na ukarabati wa sehemu zilizoharibika na uwekaji wa tabaka jipya la lami katika kipande cha kilometa 10, kuanzia Dareda hadi Masqaroda.
Kazi zinazoendelea ni pamoja na matengenezo ya viraka na maandalizi ya njia za mchepuko zitakazowezesha magari kuendelea kupita wakati wa ukarabati.
Kwa upande wa kilometa 25.8 zilizobaki kufanyiwa ukarabati, mkandarasi aliyepata zabuni anaendelea na maandalizi ya kupeleka mitambo, vifaa na rasilimali nyingine katika eneo la mradi kabla ya kuanza kwa utekelezaji.
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Manyara imeeleza kuwa itaendelea kusimamia utekelezaji wa kazi hizo ili kuhakikisha zinazingatia viwango vya ubora, masharti ya mikataba na muda uliopangwa, huku usalama wa watumiaji wa barabara na wananchi wanaoishi maeneo jirani ukizingatiwa.
Aidha, watumiaji wa barabara hiyo wametakiwa kupunguza mwendo, kuzingatia alama za tahadhari na kufuata maelekezo ya usalama katika maeneo yanayofanyiwa matengenezo ili kuepusha ajali na kulinda usalama wao pamoja na wafanyakazi wa mradi.
Barabara ya Gehandu–Babati ni kiungo muhimu kati ya mikoa ya Manyara na Singida, na sehemu ya mtandao wa barabara unaorahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kuelekea maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani.