Kamati imeishauri Serikali kuweka utaratibu wa kutoza ushuru wa matumizi ya Daraja la Tanzanite ili kuongeza mapato yatakayosaidia kugharamia ujenzi wa madaraja mengine nchini. Kamati imesema hatua hiyo itasaidia kupanua wigo wa mapato ya miundombinu badala ya kutegemea fedha za bajeti pekee, huku ikiielekeza Serikali kutumia fursa hiyo kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya kukagua miradi ya miundombinu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu ,Mheshimiwa Selemani Kakoso amesema mfumo wa Road Toll unaweza kuwa chanzo muhimu cha mapato, akitolea mfano matumizi ya madaraja na barabara katika nchi mbalimbali duniani ambako watumiaji huchangia gharama za miundombinu wanayotumia.
Katika ziara hiyo, Kamati pia imekagua Daraja la Jangwani lenye uwekezaji wa Serikali wa takribani shilingi bilioni 97, na kueleza kuridhishwa na usimamizi wake, huku ikiitaka Serikali kuhakikisha mkandarasi anakamilisha mradi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa kwenye mkataba.
Aidha, Kamati imeeleza kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), ambayo imekuwa ikisuasua, na kuitaka Serikali kuondoa changamoto zinazokwamisha kazi, ikiwemo uhamishaji wa mabomba ya maji na nyaya za umeme, kuongeza usimamizi kwa wakandarasi na kuchukua hatua za kimkataba, ikiwemo kudai fidia pale masharti ya mikataba yanapokiukwa.
Vilevile, Kamati imeishauri Serikali kuhakikisha miradi mikubwa ya miundombinu inaacha manufaa ya kudumu kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya utekelezaji kupitia Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), ikipendekeza ujenzi wa shule na vituo vya afya kama sehemu ya kurejesha manufaa kwa jamii zinazotoa maeneo na ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo.