News

WAKANDARASI WAAGIZWA KUONGEZA KASI JANGWANI NA MIRADI YA BRT

Serikali imeeleza kuwa inaendelea kuchukua hatua za kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Daraja la Jangwani jijini Dar es Salaam, baada ya kubainika kuwepo kwa tofauti ya maendeleo kati ya miradi hiyo inayotekelezwa na wakandarasi wawili tofauti, ambapo mradi mmoja umefikia zaidi ya asilimia 70 huku mwingine ukiwa katika kiwango cha takribani asilimia 46.

Akieleza Naibu Waziri wa Ujenzi  Mheshimiwa Godfrey Kasekenya, amesema baadhi ya wakandarasi wamekumbana na changamoto za miundombinu iliyopo katika maeneo ya ujenzi, huku wengine wakichelewa kuanza kazi kutokana na maandalizi na uhamasishaji wa rasilimali hali iliyochangia kutofautiana kwa kasi ya utekelezaji.

Amefafanua kuwa Serikali imeelekeza wakandarasi kuongeza wataalamu na mitambo pamoja na kutumia muda wa nyongeza waliopatiwa ili kuhakikisha kazi zilizochelewa zinaongezewa kasi na kukamilika kwa wakati.

Aidha, Serikali imepokea ushauri na maelekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge na kuahidi kuyafanyia kazi, ikisisitiza kuwa jukumu la Bunge ni kuishauri na kuielekeza Serikali, huku Serikali ikiwa na wajibu wa kutekeleza maelekezo hayo kwa kuweka mikakati na hatua stahiki.