News

MABOMBA YA PLASTIKI, MADARAJA YA CHUMA YAWEKWA TAYARI KUKABILIANA NA ATHARI ZA MVUA NA MAFURIKO MTWARA

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mtwara imejiandaa kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa za El Niño kwa kuweka vifaa na miundombinu mbadala itakayosaidia kurejesha mawasiliano endapo barabara na madaraja vitaharibiwa na mafuriko.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mhandisi wa miradi Michael Nkya wa TANROADS Mkoa wa Mtwara amesema, wakala huo umenunua mabomba ya plastiki yenye urefu wa jumla ya mita 154 ambayo yamewekwa katika maeneo ya Lindi na Masasi, pamoja na kuandaa daraja la chuma maarufu kama Bailey Bridge kwa ajili ya kukabiliana na dharura.

Amesema daraja hilo limeandaliwa ili kusaidia kurejesha mawasiliano ndani ya saa 24 hadi 36 endapo kutatokea uharibifu wa miundombinu ya barabara unaosababisha kukatika kwa huduma za usafiri.

Aidha, amesema TANROADS imeweka wahandisi katika kila wilaya watakaokuwa tayari kufanya doria na kufuatilia hali ya barabara ili kubaini changamoto na kuzishughulikia kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Nkya amesema, mkoa huo una zaidi ya madaraja 210 kwenye barabara kuu, ambapo kati ya hayo asilimia 90 hadi 98 yamefunguliwa, huku kazi ya kusafisha mitaro na makalavati ikiendelea ili kuruhusu maji kupita bila kuziba njia za maji.

Amewataka wananchi kushiriki katika kulinda miundombinu hiyo kwa kutoa taarifa mapema wanapoona changamoto yoyote inayohusiana na barabara au madaraja kupitia ofisi za Serikali zilizo karibu nao, ili hatua za haraka zichukuliwe