News

TANROADS RUVUMA YAONYA VITENDO VYA UHARIBIFU WA MIUNDOMBINU KUKABILIANA NA EL NINO.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Salehe Juma amewataka wananchi hususani wanaojishughulisha na kilimo kuacha tabia ya kulima pembezoni mwa barabara na kwenye maeneo yaliyo karibu na mikondo ya maji na kusisitiza kuwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na vinagharimu usalama wa barabara.

Akizunguza mara baada ya ziara yake ya kukagua miundombinu ya barabara zinazotengenezwa katika hatua ya kukabiliana na mvua za El Nino, Mhandisi  Salehe amesema katika baadhi ya maeneo ikiwemo makutano ya Hospitali ya Peramiho na Kingole, Mazimbu na Barabara ya Litura kuelekea Kitui hadi Mbamba Bay baadhi ya barabara zake zimeathirika kutokana shughuli za kilimo zisizozingatia sheria ya uhifadhi wa barabara.

Ameongeza kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa Mkoa wa Ruvuma kiuchumi katika sekta ya kilimo na usafirishaji wa makaa ya mawe, wananchi wanapaswa kuzitunza barabara hizo zilizojengwa na serikali kwa mabilioni ya fedha ili ziwasaidie kuongeza kasi ya maendeleo.

Mhandisi Salehe amesema  baada ya timu ya wataalamu kutoka TANROADS kufanya ukaguzi na kubaini maeneo 12 ambayo miundombinu yake ya barabara ilikuwa hatarini iliweka mpango kazi wa kuiboresha kwa kujenga makaravati, kufungua mifereji, kusafisha njia za kuingiza na kutoa maji na kurekebisha barabara zilizoko maeneo ambako shughuli za kilimo zinaendeshwa ili kupunguza uwezekano wa maji kujaa na kuharibu barabara hatua ambayo amesema imeonyesha mafanikio kwa sasa maji yatapita wakati wote bila kikwazo.

Kuhusu suala la usalama wa watumiaji wa barabara na madereva wakati wa kipindi cha mvua, Mhandisi Salehe amewaasa kuepuka kuvuka maeneo yenye maji mengi wanayoyatilia mashaka badala yake wawe na Subira mapaka maji yatakapokwisha au watoe taarifa TANROADS ili wataalamu wake waweze kuchukua hatua kubaini ukubwa wa tatizo.

Pia mhandisi Salehe amewataka wakazi wa mkoa wa Ruvuma kushirikiana na TANROADS kulinda miundombinu ya barabara hizo ili ziweze kupitika wakati wote bila kuathiri shughuli za kiuchumi.