News

TANROADS YAJA NA MIKAKATI BUNIFU YA KUPUNGUZA FOLENI BARABARA YA TANGA–SEGERA–CHALINZE

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tanga imeweka mikakati mbalimbali ya kupunguza foleni na misongamano ya magari katika barabara ya Tanga–Segera–Chalinze, ikiwemo ujenzi wa njia za maegesho na njia maalumu za kupandia milima katika maeneo yenye changamoto.

Mikakati hiyo inalenga kurahisisha mtiririko wa magari, kupunguza muda wa safari na kuzuia malori yanayosimama au kupanda milima kwa mwendo mdogo kusababisha msongamano kwa watumiaji wengine wa barabara.

Akizungumza kuhusu hatua hizo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama Kosani Msama, amesema Wakala imeanza kuchukua hatua za kuboresha barabara hiyo kutokana na umuhimu wake katika usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Tanga kwenda maeneo mbalimbali ya nchi.

Amesema njia za maegesho (parking lanes) zimewekwa ili kuruhusu magari kusimama bila kuzuia mtiririko wa magari mengine, huku njia za kupandia milima (climbing lanes) zikisaidia magari yanayotembea kwa mwendo mdogo kupisha magari mengine, hususan katika maeneo korofi kama Mambo Leo.

Mhandisi Msama ameongeza kwa kusema kuwa, TANROADS pia inaendelea kupanga na kutekeleza mikakati ya kuongeza njia hizo katika maeneo mbalimbali yenye miinuko kuanzia Tanga, Segera hadi maeneo ya Mkoa wa Pwani, kulingana na upatikanaji wa fedha.

Aidha, ameshukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zinazowezesha utekelezaji wa mipango ya kuboresha miundombinu ya barabara.

Ameeleza kuwa kupunguza foleni katika barabara hiyo kutasaidia kuboresha usafirishaji wa mizigo, kulinda maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi. Katika hatua nyingine, amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwa makini ili kuepusha ajali na misongamano inayoweza kuzuilika.