Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi imeimarisha maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua zitakazoambatana na Hali ya za El Niño zinazotarajiwa kunyesha kuanzia Novemba hadi Februari, kwa kufanya usafi wa mitaro na madaraja pamoja na kusambaza vifaa vya dharura katika maeneo hatarishi.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Ezra Mwagogo Daniel, amesema ofisi yake imefanya usafi wa mitaro ya barabarani na kusafisha madaraja ili kupunguza uwezekano wa uharibifu wa miundombinu wakati wa mvua hizo.
Amesema maeneo yaliyofanyiwa usafi ni pamoja na Madaraja ya Mtange, Ngongo, Tulieni, Sandamkobani na Kilangala II, hatua inayolenga kuboresha upitishaji wa maji na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa.
Ameongeza kuwa makalvati ya plastiki yamewekwa katika eneo la Mizani wa Nangurukuru, huku makalvati ya chuma yenye urefu wa jumla ya karibu mita 200 yakisambazwa katika vituo vya Nachingwea mjini na Liwale kwa ajili ya kurahisisha hatua za dharura pale changamoto zitakapojitokeza.
Aidha, amewataka wananchi kuchukua tahadhari wanapotumia barabara wakati wa mvua, hususani katika maeneo ambayo maji yanaweza kufurika na kufunika barabara, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa za dharura kwa viongozi wa serikali za mitaa na vijiji inapotokea changamoto.