News

TANROADS TANGA YAENDELEA KUJIANDAA KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NIÑO, YAFANYA UKAGUZI WA BARABARA

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Tanga imeimarisha maandalizi ya kukabiliana na mvua za El Niño kwa kufanya ukaguzi wa kina katika barabara zote saba za mkoa huo, kubaini maeneo hatarishi na kuchukua hatua za kuzuia uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Tanga, Mhandisi Msama Kosani Msama, amesema baada ya kupokea taarifa za mvua hizo, wataalamu wa wakala walifanya tathmini katika wilaya zote saba za mkoa ili kubaini maeneo yanayoweza kuathiriwa na mvua kubwa.

"Baada ya hapo tulianza mara moja kwenda kutambua maeneo ambayo ni ya hatari kwenye mkoa wetu. Tulipita mkoa wote, wilaya zote saba za mkoa wa Tanga na tuliweza ku-identify maeneo mengi ambayo ni ya hatarishi," amesema Mhandisi Msama.

Amesema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuziba nyufa kwenye barabara za lami, kufanya portal patching (kurekebisha sehemu ya barabara iliyoharibika), pamoja na kusafisha madaraja na makalvati ili kuhakikisha maji yanapita kwa urahisi bila kusababisha uharibifu wa miundombinu.

Mhandisi Msama ameishukuru Serikali kwa kuwezesha maandalizi hayo kupitia upatikanaji wa vifaa vinavyohitajika.

"Kwa maandalizi ambayo tumekwisha yafanya kusema ukweli lazima niishukuru sana Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu wametupa vifaa, wametuandalia, tumeweza kufanya maandalizi kwa ajili ya hizi mvua za El Niño," amesema.

Ameongeza kuwa TANROADS inaendelea kushirikiana na wakandarasi waliopo katika maeneo ya kimkakati, pamoja na TARURA, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Polisi na mamlaka za mkoa, ili kuhakikisha hatua za dharura na uokoaji zinachukuliwa kwa wakati endapo mvua hizo zitasababisha athari.