Ujumbe wa Benki ya Dunia, ukiambatana na Meneja wa Miradi ya Tanzania Transport Integration Project (TanTIP) pamoja na wasimamizi kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), umetembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Iringa–Msembe kwa lengo la kukagua kazi zinazotekelezwa na kujionea maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo.
Katika ziara hiyo, ujumbe ulipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Mshauri kuhusu usanifu wa barabara hiyo, ambapo kipande cha mwanzo chenye urefu wa kilomita 1.5 kitajengwa kwa kiwango cha barabara ya njia nne, huku kipande cha Mwangata hadi Kalenga chenye urefu wa kilomita 11 kikiwa na njia mbili za magari pamoja na njia za bajaji pembeni. Sehemu iliyobaki hadi mwisho wa mradi itakuwa na njia mbili za magari.
Aidha, mkandarasi amekamilisha ujenzi wa makalavati madogo 130 na makalavati makubwa 33, huku kazi za ujenzi wa madaraja matatu zikiendelea katika maeneo ya Kalenga lenye urefu wa mita 60, Mlowa lenye urefu wa mita 20 na Tungamalenga lenye urefu wa mita 60.
Ujumbe wa Benki ya Dunia umepongeza kazi zilizofanyika na zinazoendelea kutekelezwa katika mradi huo, huku ukisisitiza mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi ili kuhakikisha utekelezaji unaendelea kwa kuzingatia viwango vya ubora na masharti ya mkataba.
Mradi wa barabara ya Iringa–Msembe ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kurahisisha safari za kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kuimarisha shughuli za utalii katika eneo hilo.