News

TANROADS YAIMARISHA MAANDALIZI YA MIRADI KWA KUONDOA VIZUIZI KWENYE HIFADHI ZA BARABARA

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuondoa vizuizi na shughuli za kibiashara zisizo na vibali katika hifadhi za barabara ili kuwezesha maandalizi na utekelezaji wa miradi ya ujenzi na upanuzi wa barabara nchini.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, amesema matumizi ya hifadhi za barabara yanapaswa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa, huku shughuli zinazohitaji vibali zikiendeshwa kwa kufuata taratibu husika.

Amesema zoezi hilo linahusisha maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, yakiwemo barabara ya Mwaikibaki, Mbagala - Uwanja wa Azam, Chamazi na Mbezi - Victoria - Bunju, ambako maeneo ya hifadhi yanahitajika kuwa wazi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi husika.

Aidha, amewahimiza wananchi wanaohitaji kutumia hifadhi za barabara kwa shughuli zinazoruhusiwa kuwasilisha maombi na kufuata taratibu za kupata vibali.

Vibali hivyo hutolewa kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa, ikiwemo kuachia eneo linapohitajika kwa ajili ya maendeleo ya barabara, na vina muda maalumu wa matumizi.

TANROADS inawasihi wananchi kushirikiana na Wakala kwa kuondoa vizuizi na kuepuka shughuli zisizo na vibali katika hifadhi za barabara ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya miundombinu ya barabara.