News

TANROADS YATIA SAINI MKATABA WA SHILINGI BILIONI 59.49 KUTEKELEZA UJENZI WA MIFEREJI KATIKA ENEO LA TEGETA, BOKO - BASIHAYA, DAR ES SALAAM.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini Mhandisi Mohamed Besta ameiagiza Kampuni ya China Gezhouba Group ya China kuhakikisha inazingatia makubaliano yaliyomo kwenye mkataba wa ujenzi wa mradi wa miundombinu ya maji ya mvua katika barabara ya Bagamoyo eneo la Boko - Basihaya ikiwemo matumizi ya vifaa vya kisasa.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 59.49 mjini Dodoma, Mhandisi Besta amesema utekelezaji wa mradi huo ni kielelezo cha jitihada za serikali katika kuboresha miundombinu ya barabara nchini ili kuruhusu shughuli za maendeleo kufanyika wakati wote.

Aidha Mhandisi Besta amemweleza mwakilishi wa Kampuni ya China Gezhouba Group, Zhou Daifei kuwa kiu ya wakazi wa eneo la Boko - Basihaya ni kuona mradi huo unakamilika ndani ya miezi 14 iliyoainishwa kwenye mkataba hatua itakayowasaidia kuondokana na adha ya ukosefu wa mifereji ya kupeleka maji baharini ambayo imekuwa ikiathiri shughuli za maendeleo.

" Ndugu Mwakilishi wa Kampuni ya China Gezhouba Group, nikuhakikishie TANROADS ikiwa ni taasisi yenye dhamana ya kusimamia mradi huu tutawapa ushirikiano wakati wote, ni matarajio yetu mradi huu utatekelezwa katika viwango vya ubora kama ilivyoainishwa kwenye mkataba" alisisitiza Mhandisi Mohamed Besta.

Kwa upande wake, mwakilishi wa kampuni hiyo Zhou Daifei ameishukuru serikali kwa kuipatia nafasi ya kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo huku akiahidi kuusimamia kikamilifu ili uweze kutoa matokeo chanya.

Utekelezaji wa mradi huo utakaohusisha uhamishaji wa miundombinu ya maji unatarajiwa kuanza hivi karibuni.