News

TAA 400 ZA BARABARANI GEITA ZAIMARISHA USALAMA NA KUKUZA BIASHARA

Taa 400 za barabarani zilizowekwa kuanzia Mwatolole hadi Nyankumbu na maeneo mengine mkoani Geita zimelezwa kuimarisha usalama wa madereva na wananchi nyakati za usiku, huku wafanyabiashara wakieleza kuwa zimewawezesha kuongeza muda wa kufanya biashara.

Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Geita, Mhandisi Hosea Machaka, amesema uwekaji wa taa hizo ni muhimu hasa katika kipindi cha mvua, kwa kuwa zinasaidia madereva kuona vizuri na kuongeza usalama kwenye barabara yenye matumizi makubwa ya magari.

Ameongeza kwa kusema kuwa, uwekaji wa taa hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupitia TANROADS wa kupendezesha miji, kuimarisha usalama na kuchochea shughuli za kiuchumi na usafirishaji.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Machaka amewataka wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma na kuchangia usalama pamoja na maendeleo ya kiuchumi.

Kwa upande wake mfanyabiashara na mkazi wa Shilabela, Peter Kurwa maarufu Wandonga, amesema taa hizo zimebadili mazingira ya biashara eneo hilo, akieleza kuwa awali walilazimika kufunga biashara mapema kutokana na giza.

“Toka tuanze kufanya hapa biashara kipindi cha nyuma tulikuwa tunafanya biashara kwa giza kwa sababu barabara ilikuwa haina mataa, ila tangu yawekwe mataa ah saivi tunafanya biashara vizuri,” amesema Kurwa.

Amesema kutokana na uwepo wa taa hizo, sasa anaweza kuuza matunda hadi saa 5:00 au 6:00 usiku, tofauti na awali ambapo biashara zilimalizika majira ya saa 3:00 usiku.

Kwa upande wake, Afisa Usafirishaji, Novatus Amina, amesema taa hizo zimeondoa changamoto ya kufanya kazi na kutembea gizani, na kuwawezesha kuendelea na shughuli za usafirishaji kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 6:00 usiku na wakati mwingine kukesha.