Utekelezaji wa ujenzi wa Daraja hilo umeendelea kupewa msukumo kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam, huku usimamizi mzuri wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ukipongezwa na Serikali kwa kuhakikisha kazi zinaendelea kwa kasi na kuzingatia ubora.
Akizungumza wakati wa kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amesema mradi huo ulipokelewa kwa shangwe na wananchi wakati Mheshimiwa Rais alipouzungumzia mwanzoni mwa kampeni, akieleza kuwa utekelezaji wake ni sehemu ya uwekezaji mkubwa unaoendelea katika miundombinu ya Dar es Salaam.
Amesema pamoja na ujenzi wa daraja hilo, Serikali inaendelea na miradi mbalimbali ikiwemo upanuzi wa barabara, ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka pamoja na maandalizi ya miradi ya reli na barabara zitakazosaidia kuunganisha maeneo mbalimbali na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Mhe. Kadogosa ameipongeza TANROADS kwa usimamizi wa mradi huo, akisema ubora unaoonekana katika utekelezaji wake unatokana na usimamizi mzuri unaofanywa na wahandisi, washauri na viongozi wa Wakala ya barabara. Amesema kukamilika kwa kazi za piling mapema ni hatua muhimu kwa kuwa kunapunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua wakati wa kuendelea na ujenzi.
Aidha, amemtaka Meneja wa Mradi kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa mujibu wa mkataba ifikapo Desemba 2027, huku akieleza kuwa kutokana na kasi ya utekelezaji, kuna uwezekano wa mradi kukamilika hata kabla ya muda uliopangwa.
Mhe. Kadogosa amesema Serikali inaendelea kuweka mkazo katika ujenzi na matengenezo ya miundombinu kwa kuwa miundombinu ni msingi wa uchumi, kwani usafirishaji wa watu na bidhaa kutoka eneo moja kwenda jingine unategemea uwepo wa barabara na madaraja yanayopitika kwa uhakika.
Amesema Serikali pia inaendelea na maandalizi ya kuhakikisha njia muhimu za usafirishaji, ikiwemo kutoka Dar es Salaam kuelekea bandari na nchi jirani, zinaendelea kuwa salama na kupitika wakati wote.