Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya imeanza kuchukua hatua za kuimarisha maeneo hatarishi kwenye barabara zake kuelekea msimu wa mvua za El Niño, kwa kuweka tabaka la zege katika maeneo yenye miteremko na utelezi mkubwa.
Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Mhandisi Doris Mwaipaja, amesema maeneo yaliyotambuliwa kuwa na vihatarishi ni pamoja na barabara ya Isyonje–Kikondo yenye urefu wa kilomita 21.99 na barabara ya Mbeya–Rungwa yenye urefu wa kilomita 288.89, hususan kipande cha Mbeya–Chunya cha kilomita 70.7.
Amesema barabara ya Isyonje–Kikondo ina milima, miteremko na utelezi mkubwa, hali inayoweza kuathiri usalama na upitishaji wa magari wakati wa mvua, hivyo TANROADS imeanza matengenezo katika maeneo ya Mlima Idi na Mlima Nyalwela kwa kuweka tabaka la zege imara.
Vilevile amesema TANROADS imejipanga kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote wa msimu wa mvua, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa haraka katika ofisi za Serikali zilizo karibu pindi wanapoona changamoto kwenye barabara au madaraja.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi huo, Mhandisi Debora Kabendile, amesema matumizi ya zege yanalenga kutoa suluhisho la muda mrefu kwa maeneo hatarishi, hasa kwenye kona, kwa kuwa ni imara zaidi ikilinganishwa na lami iliyokuwepo awali.
Amesema barabara hiyo ina umuhimu wa kimkakati kwa kuwa inaunganisha maeneo yanayofika hadi Singida na Tabora, huku ikiwahudumia wakulima wa tumbaku na wachimbaji wa madini katika eneo la Chunya.
Naye , Mkurugenzi wa Mwendokasi Construction bad General Enterprises Ltd, Deonis Kiyombo, amesema kampuni hiyo imepewa tenda ya kujenga na kusimamia barabara hiyo kipindi cha mvua za El Niño, ikiwa tayari kutoa ushirikiano na kuhakikisha matengenezo yanaendelea wakati wote.