Maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Awamu ya Nne sehemu ya kwanza, (BRT 4 - 1) jijini Dar es Salaam yamefikia asilimia 65, huku kazi mbalimbali zikiendelea katika maeneo tofauti ya mradi.
Akizungumza kuhusu maendeleo hayo, Mhandisi Justin Moshi, Meneja Msaidizi wa Mradi wa BRT Awamu ya Nne sehemu ya kwanza, amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara maalum za BRT pamoja na barabara za magari mchanganyiko zenye urefu wa jumla ya kilomita 13.5, zinazounganisha maeneo ya CBD Maktaba ya Taifa, Mwenge, Sam Nujoma Road na Kijazi Interchange.
Amesema miongoni mwa kazi muhimu zinazoendelea ni ujenzi wa Daraja la Salender, ambalo litakapokamilika litasaidia kurahisisha mtiririko wa magari kutoka katikati ya jiji kuelekea Kinondoni na Ubungo. Aidha, mradi unahusisha ujenzi wa vituo 20 vya BRT, ambapo ujenzi umefikia asilimia 77 na kazi za misingi zimekamilika kwa asilimia 100, huku kazi zinazoendelea zikihusisha ujenzi wa sehemu za juu, miundombinu ya chuma, kuezeka na ukamilishaji. Pia, kati ya vituo 11 vya mabasi feeder, vituo nane vimefikia takribani asilimia 95.
Mhandisi Moshi amesema changamoto mojawapo katika utekelezaji wa mradi ni msongamano wa magari unaosababishwa na kazi za ujenzi katika maeneo yenye shughuli nyingi, huku Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ikiendelea kuchukua hatua mbalimbali kupunguza usumbufu kwa watumiaji wa barabara kwa kutoa taarifa endapo barabara ikifungwa kwa matumizi huku Ujenzi ukiendelea.
Amewataka watumiaji wa barabara kuwa na subira, kuzingatia alama za barabarani pamoja na maelekezo wanapopita katika maeneo ya ujenzi kwa ajili ya usalama na kurahisisha mtiririko wa magari. Aidha, amesema mradi huo umeendelea kutoa fursa za ajira na shughuli za kiuchumi kwa wananchi, wakiwemo wafanyabiashara wadogo, na kwamba utakapokamilika unatarajiwa kusaidia kupunguza msongamano wa magari na kuboresha huduma za usafiri wa umma jijini Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine, mradi huu umetoa fursa mbalimbali kwa vijana na wananchi, ikiwemo ajira na fursa za kiuchumi. Pia, wafanyabiashara wadogo, wakiwemo wamachinga, wameweza kupata fursa za kuendesha biashara zao katika maeneo yanayohusiana na mradi.