Dodoma: Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, amesema kazi za ujenzi na uboreshaji wa Barabara ya Kikombo kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Usafirishaji Dodoma (TPDP) zinaendelea kwa kasi, huku hatua zikichukuliwa kuhakikisha barabara hiyo inakuwa salama wakati wa msimu wa mvua.
Mhandisi Zuhura amesema kazi ya kujaza kifusi nyuma ya madaraja (backfilling) imekamilika katika madaraja ya Mwitikila, Mangungo na Kikombo.
Amesema kwa sasa mkandarasi anaendelea na kazi za kuelekeza mkondo wa maji (river training) pamoja na kuondoa nguzo na vifaa vya muda vilivyotumika wakati wa ujenzi wa madaraja hayo.
“Tumemwelekeza kuhakikisha maeneo ya maungio kati ya barabara na madaraja yanajazwa vizuri ili kusiwe na mwinuko au mteremko unaoweza kuathiri usalama wa watumiaji,” amesema Mhandisi Zuhura.
Aidha, amesema mkandarasi ameelekezwa kuhakikisha kingo za madaraja zinalindwa ipasavyo ili kuzuia mmomonyoko wa udongo unaoweza kusababishwa na maji ya mvua.
Amesema magari yanaendelea kutumia barabara hiyo wakati kazi zikiendelea, huku kazi ya kujaza tuta katika maeneo ya madaraja ya MGR na SGR ikiendelea.
“Kazi ya kujaza tuta bado ni kubwa, lakini haitawaathiri watumiaji kwa sababu kuna barabara mbadala inayopita kijijini ambayo tunaendelea kuimarisha,” amesema.
Kuhusu ukamilishaji wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, Mhandisi Zuhura amesema utekelezaji wa hatua hiyo unategemea upatikanaji wa malipo yaliyobaki ya madai ya kazi.
Hata hivyo, amesema mkandarasi anaendelea kutekeleza kazi muhimu zilizoelekezwa, hususan zile zinazolenga kuhakikisha barabara na madaraja yanakuwa salama na kuhimili athari za mvua.