Ujumbe wa Benki ya Dunia umefanya ziara Mkoani Rukwa kwa ajili ya ukaguzi wa mwisho wa utekelezaji wa miradi ya dharura chini ya mpango wa CERC, huku Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ikieleza kuwa imeweka mikakati kuhakikisha madaraja na barabara zake zinakuwa salama dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua kubwa za El Niño.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhandisi Mkuu wa Kitengo cha Ushauri wa Kihandisi cha TANROADS (TECU), Mhandisi Lutengano Mwandambo, amesema timu hiyo imekagua ubora wa miundombinu iliyojengwa pamoja na kazi za ulinzi zinazolenga kuongeza uwezo wa madaraja na barabara kuhimili mvua kubwa.
Amesema mkoani humo kuna mradi mmoja wa CERC unaohusisha ujenzi wa madaraja matatu ya Ilemba, Kinambo na Kisa, huku ukaguzi ukilenga pia kuhakikisha kazi za ulinzi wa miundombinu hiyo zimefanyika kwa ubora unaohitajika.
Mhandisi Mwandambo ameendelea kwa kusema kuwa, TANROADS inalenga kukamilisha kazi zote ndani ya muda uliowekwa, kabla ya kufungwa kwa dirisha la miradi hiyo ya dharura.
Aidha, ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutafuta fedha za kukabiliana na athari za mafuriko, pamoja na Benki ya Dunia kwa ufadhili wa miradi hiyo.