News

BENKI YA DUNIA YAKAGUA MIRADI YA MADARAJA RUKWA, TANROADS MBIONI KUONGEZA MADARAJA MENGINE MAWILI

Ujumbe wa Benki ya Dunia umefanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa madaraja katika barabara ya Kasansa–Muze–Kilyamatundu, huku Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Rukwa ikiweka mikakati ya kujenga madaraja mengine mawili ya Lwanji na Sakalilo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Christopher Saul, amesema barabara hiyo iliyopo pembezoni mwa Ziwa Rukwa imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa za mafuriko yanayotokana na maji kutoka Milima ya Ufipa, hali iliyokuwa ikisababisha barabara kukatika na kusomba tuta pamoja na madaraja.

Amesema Benki ya Dunia imefadhili ujenzi wa madaraja makubwa matatu kupitia mfuko wa dharura wa CERC, ambayo ni Daraja la Ilemba lenye urefu wa mita 60, Kinambo mita 50 na Kisa mita 40.

Akifafanua zaidi Mhandisi Saul amesema, ujenzi wa madaraja hayo ulianza Desemba 2024 na kukamilika Februari 2026, huku ujenzi wa barabara za maingilio ukikamilika Septemba 2026.

Ameongeza kwa kusema kuwa, kazi ndogo zilizobaki, ikiwamo ujenzi wa gabions na reno mattresses (makasha ya nyavu za waya yaliyojazwa mawe kwa ajili ya kuimarisha kingo za daraja na kuzuia mmomonyoko) na ufungaji wa taa, zinatarajiwa kukamilika ndani ya mwezi mmoja.

Vilevile amesema, TANROADS ipo katika mpango wa kujenga madaraja mawili zaidi kupitia mfumo wa CRW, ambayo ni Lwanji lenye urefu wa mita 200 na Sakalilo lenye mita 80, hatua itakayofanya jumla ya madaraja mapya katika eneo hilo kufikia matano.

“Pamoja na hayo, kukamilika kwa madaraja haya matatu ambayo nimeyataja, imekuwa na manufaa makubwa sana kwa wakazi wa Mkoa wa Rukwa kwa sababu maeneo yale ambayo yalikuwa korofi sasa yatakuwa yanapitika kwa urahisi na wananchi wataweza kufurahia matunda ya serikali yao,” amesema.