Mhandisi Hamza Faiswary kutoka Wakala ya Barabara Tanzania TANROADS Makao Makuu na Mratibu wa Mradi wa Ushirikiano wa Usafiri Tanzania (Tanzania Transport Integration Project - TanTIP), amesema hatua zilizochukuliwa katika ukarabati na ujenzi wa madaraja yaliyoharibiwa na mafuriko mkoani Morogoro zitasaidia kuzuia madhara endapo mvua zitaanza kunyesha tena.
Mhandisi Faiswary amesema hayo wakati wa ziara ya ujumbe wa Benki ya Dunia ya kukagua utekelezaji wa miradi ya dharura iliyoibuka baada ya mvua za El Niño na mafuriko yaliyosababisha kuharibika kwa miundombinu ya barabara na madaraja.
Amesema mradi wa TanTIP, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, unahusisha ujenzi na ukarabati wa barabara katika maeneo mbalimbali nchini, zikiwemo kilomita 92 mkoani Kagera, kilomita 104 Iringa, kilomita 201 Mtwara na kilomita 416 Songea, pamoja na viwanja vitatu vya ndege vya Iringa, Tanga na Lake Manyara.
Kwa upande wa Morogoro, amesema madaraja yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na Doma, Ngerengere, Kihonda, Nguyami, Bwage, Ijonga na Chapwera, ambapo miradi mingi imekamilika huku baadhi ikiwa katika hatua za mwisho.
Akizungumzia hali ya madaraja hayo, Mhandisi Faiswary amesema hatua zilizofikiwa zinatoa uhakika wa usalama wa miundombinu hiyo wakati wa mvua zijazo.
Baada ya kukamilisha ukaguzi mkoani Morogoro, ujumbe huo wa Benki ya Dunia na TANROADS utaendelea na ziara maalum mkoani Rukwa na baadaye Lindi na Mtwara kwa ajili ya kukagua miradi mingine ya dharura inayotekelezwa chini ya TanTIP.
Mradi wa TanTIP (Tanzania Transport Integration Project) ni mradi mkubwa wa kimkakati unaotekelezwa na Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (World Bank) ili kuboresha mtandao wa usafiri na miundombinu nchini.